Na.Sophia Kingimali.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua mfumo mpya wa kupokea taarifa za siri unaofahamika kama Whistle blower wenye lengo kudhibiti vitendo vya uhalifu, rushwa, na uharibifu wa miundombinu ya umeme lakini pia utakaoweza kutumika na wafanyakazi wa shirika kuripoti matendo ya ukatili wa kijinsia wanayokutana nayo kwenye utendaji wao.
TANESCO pia inaendelea na kampeni ya kitaifa ya “Lipa Deni Tukuhudumie”, inayolenga kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa wakati kwa wananchi wote.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele, amesema mfumo huo wa Whistleblower Portal ni hatua ya kimageuzi katika utendaji wa shirika hilo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukikumbwa na changamoto kama vile wizi wa miundombinu ya umeme na vitendo vya rushwa kutoka kwa baadhi ya watumishi. Mfumo huu mpya utarahisisha upokeaji wa taarifa na kulinda usalama wa mtoa taarifa,” amesema Gowele.
Ameeleza kuwa taarifa zitapokelewa na kushughulikiwa kwa usiri mkubwa, huku mtoa taarifa akielekezwa hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu.
Ameongeza kuwa wananchi wataweza kutumia njia mbili kuwasilisha taarifa zao kupitia tovuti ya shirika ambayo ni www.tanesco.co.tz kwa kubonyeza kiungo cha Whistleblower Portal na kujaza fomu salama na kupiga simu bila malipo kupitia namba 180, kisha kubonyeza namba 2 kuzungumza na watoa huduma wa shirika
Aidha, shirika limewahimiza wananchi kote nchini kushiriki kikamilifu katika matumizi ya mfumo huo ili kusaidia kulinda rasilimali za shirika na Taifa kwa ujumla.