Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Agosti 3, 2025
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wagombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Kibaha Mjini wameendelea na mikutano ya kujitambulisha kwa wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi, huku kila mmoja akijinadi kwa vipaumbele vyake vya kiutendaji pindi atakapopewa ridhaa.
Mgombea Mwalimu Abubakar Allawi amejitokeza na kueleza kuwa yeye ndiye mtu sahihi kwa kuleta mabadiliko kwenye jimbo hilo.
Akizungumza kwenye mikutano ya Agosti 2 na 3, katika kata za Msangani, Pangani, Mbwawa, Kongowe na Mailimoja, Allawi alisema ana ufahamu wa kina kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo.
Nae Mussa Mansour, maarufu kwa jina la Dangote, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani, aliahidi kutoa kipaumbele kwa vijana kupata mitaji ili kuanzisha miradi ya kujitegemea kwa lengo la kupunguza ukosefu wa ajira.
Mansour alieleza kuwa tayari ameanza kusaidia matawi ya chama kwa kuchangia saruji na fedha ili kusaidia ujenzi wa ofisi, baada ya kubaini uhaba mkubwa wa miundombinu hiyo.
Mbunge aliyemaliza muda wake, Silvestry Koka, alisema yapo maeneo aliyoyaweka msingi ambayo bado hayajakamilika, yakiwemo miradi ya maji, barabara, elimu na umeme, na amedhamiria kuyamalizia akiwa na uzoefu wa kutosha.
Koka aliahidi kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha zinaleta matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi, hasa kwenye huduma za msingi kama elimu, afya na miundombinu.
Wakili Magreth Mwihava aliomba apewe nafasi ya kipekee kama mwanamke kiongozi.
Alisema kuwa mwanamke akipewa nafasi ya kuongoza anaweza kusimamia vyema rasilimali za wananchi, pia akisisitiza kuwa atasimamia haki za wanawake na kutatua migogoro ya kisheria inayowakabili wakazi wa Kibaha Mjini.
Mbali na wagombea hao wengine wanaowania nafasi hiyo ni Charles Mwamwaja na Ibrahim Mkwiru, ambao wanatarajiwa kupigiwa kura na wajumbe wa kata tarehe 4 Agosti 2025 ambapo mchakato huu unalenga kumpata mgombea mmoja atakayewakilisha Chama katika Uchaguzi Mkuu ujao.