Na Meleka Kulwa – Dodoma
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa wamemchagua tena Mbunge anayemaliza Muda wake na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia kundi la watu wenye ulemavu kutoka Tanzania Bara.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, Bi. Ummy Nderiananga amepata ushindi wa kishindo kwa kujizolea kura 758, na hivyo kuibuka kinara miongoni mwa wagombea waliokuwa wakigombea nafasi hiyo muhimu ya uwakilishi wa watu wenye ulemavu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku mpinzani wake wa Karibu Stela Ikupa Alex akipata kura 708.
Zoezi la upigaji kura lilianza rasmi mnamo Agosti 2, 2025 na kufikia tamati alfajiri ya leo Agosti 3, likihitimisha hatua muhimu ya kuwapata wawakilishi wa watu kundi maalum wenye ulemavu kwa mwaka huu.
Ushindi huo unamfanya Bi. Ummy Nderiananga kutetea nafasi yake ya uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwa miaka mitano tena , kupitia ushindi huo unatoa ishara ya kuaminiwa kwake na Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) , pamoja na mchango wake katika harakati za kuwajali na kuwapambania watu wenye ulemavu ndani ya chama na jamii kwa ujumla.