Na Meleka Kulwa – Dodoma
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Bi. Mary Chatanda, amewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa jumuiya hiyo kuhakikisha wanatenda haki kwa kuwapigia kura wagombea wanaostahili na wenye dhamira ya dhati ya kukisaidia chama.
Ameyasema hayo Leo Agosti 2, 2025 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano huo maalum ulioitishwa kwa ajili ya kuchagua wawakilishi wa jumuiya hiyo watakaopata nafasi ya kuwa wabunge kupitia makundi mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia, vyuo vikuu, watu wenye ulemavu na kundi la wafanyakazi.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano huo, Bi. Mary Chatanda amewaasa kujiepusha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa uchaguzi huo unapaswa kuendeshwa kwa maadili, haki na uadilifu ili kuhakikisha viongozi bora wanapatikana.
Kwa upande mwingine amewataka wajumbe kufuata dhamira ya kweli ya kuimarisha jumuiya badala ya kujihusisha na vishawishi vinavyoweza kuvuruga mchakato wa uchaguzi na kuathiri taswira ya chama.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasisitiza wajumbe kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na chama katika mchakato wa uchaguzi.
Mongela amesema kuwa ni muhimu kwa wajumbe wote kuheshimu katiba ya chama na kuendesha uchaguzi kwa nidhamu ili kuonyesha ukomavu wa kisiasa na umoja ndani ya jumuiya.
Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini na unatarajiwa kutoa majina ya wanawake watakaowakilisha jumuiya hiyo katika nafasi za ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi.