Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu, uliofanyika leo Agosti 2, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
……
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kuhamasisha na kuelimisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu, uliofanyika leo Agosti 2, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Jaji Mwambegele amesema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa kuwapatia taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi.
Ameeleza kuwa waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kutumia taaluma yao kuwaelimisha wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili waweze kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima, amewakumbusha wanahabari kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha vyama vya siasa na wagombea wanapata nafasi ya kufikisha ujumbe wao kwa wapiga kura katika kipindi cha kampeni.
Aidha, Kailima amewataka wanahabari kutoa taarifa sahihi kwa umma na kuepuka kusambaza taarifa potofu katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na maadili ya taaluma ya habari.
Amesisitiza kuwa waandishi wanapaswa kutumia kalamu na nyenzo zao kueneza ujumbe wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ili kulinda mshikamano wa kitaifa na kuimarisha misingi ya demokrasia.
Pia amewaasa kuepuka kuchapisha au kurusha habari zinazoweza kuwakatisha tamaa wananchi na kuwafanya waone kama hakuna umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi, iwe ni kama wapiga kura au wagombea.
Mkutano kati ya Tume na Waandishi wa Habari ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wadau mbalimbali ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiitisha katika maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mikutano hiyo ilianza Julai 27, 2025 kwa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, ikafuatiwa na mkutano na wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali, kisha wawakilishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na wahariri wa vyombo vya habari.
Mfululizo huu wa mikutano unatarajiwa kuhitimishwa Agosti 4, 2025 baada ya mkutano na waandaji wa maudhui mtandaoni, utakaofuatiwa na mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari.
Katika hatua nyingine, Tume ilikumbusha kuwa utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti cha Urais na Makamu wa Rais utafanyika kuanzia Agosti 9 hadi 27, 2025.
Akitangaza tarehe hizo mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima alisema kuwa fomu za wagombea wa ubunge na udiwani zitatolewa kuanzia Agosti 14 hadi 27, 2025.
Kailima aliongeza kuwa Agosti 27 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Urais na Makamu wa Rais, pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani.
Kwa upande wa kampeni, Kailima alieleza kuwa kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara zitaanza Agosti 28 na kumalizika Oktoba 28, 2025.
Kwa upande wa Zanzibar, kampeni zitafanyika kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 27, 2025 ili kupisha siku ya upigaji kura ya pamoja itakayofanyika Oktoba 29, 2025.
Aidha, aliwaonya wagombea wanaotumia lugha ya matusi katika kampeni kuwa makini, kwani sheria itachukua mkondo wake dhidi ya vitendo hivyo.