Na John Bukuku
DAR ES SALAAM, Agosti 2, 2025
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Zena Said, amesema kuwa zaidi ya miaka kumi na mitano iliyopita, Serikali ya Tanzania ilitambua umuhimu wa uongozi na maendeleo ya uongozi katika kuleta maendeleo endelevu nchini, na hivyo kuanza kuchukua hatua madhubuti kuanzisha kituo maalum cha kushughulikia masuala hayo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kwanza ya wahitimu wa UONGOZI Institute yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mhandisi Zena alisema kuwa kupitia Mchakato wa Helsinki, ambapo ilipendekezwa kuanzishwa kwa kituo cha kikanda cha kukuza maendeleo ya uongozi barani Afrika, Tanzania iliona fursa hiyo kama ya dhahabu na kuchukua jukumu hilo kwa niaba ya Afrika.
“Tuliona huu kama wakati wa dhahabu wa kusukuma mbele ajenda ya uongozi, na Tanzania ikachukua jukumu hilo kwa ujasiri,” alisema Mhandisi Zena.
Alieleza kuwa katika safari hiyo, Serikali ya Finland imekuwa mshirika mkuu wa maendeleo, na msaada wake umekuwa wa maana kubwa katika kufanikisha shughuli za Taasisi hiyo kwa kipindi chote cha miaka kumi na mitano.
“Ningependa kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Finland kwa msaada wake wa miaka kumi na mitano. Mchango wao endelevu umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Taasisi,” aliongeza.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuishukuru Umoja wa Ulaya kwa kuwezesha kupanuka kwa Mpango wa Uongozi wa Wanawake ambao umekuwa ukitekelezwa na Taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Mhandisi Zena alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake, UONGOZI Institute imejipambanua kuwa kinara wa kukuza uongozi wenye mwelekeo wa maendeleo endelevu barani Afrika.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikilenga kuwawezesha viongozi wa Afrika kuleta mabadiliko chanya, kuchochea ubunifu, na kujenga mazingira ambayo kila mmoja anathaminiwa na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
Akizungumzia kuhusu jumuiya ya wahitimu wa taasisi hiyo (alumni), Mhandisi Zena alisema kuwa wahitimu wa UONGOZI wanajumuisha zaidi ya watu 865 kutoka sekta mbalimbali za bara la Afrika, jambo ambalo linaakisi nguvu ya utofauti wa kijinsia, sekta, utaifa na tamaduni.
“Kinachonivutia zaidi kuhusu wahitimu wa UONGOZI ni utofauti wao. Utofauti huu unaongeza thamani kwa kutoa mitazamo mipya, kuvunja dhana potofu na kuleta fursa mpya za ukuaji na ubunifu,” alisema.
Amesema Miongoni mwa faida za utofauti huo zilizobainishwa ni pa. ona na Mtazamo wa kimataifa, Uelewa wa tofauti za kitamaduni katika biashara, Kuthamini mitindo tofauti ya uongozi, Mageuzi ya binafsi, Mageuzi ya kitaaluma, na Kufikiri kwa ubunifu.
Mhandisi Zena aliwapongeza wahitimu wa taasisi hiyo kwa mafanikio yao binafsi na kuwahimiza kuendeleza maadili ya uongozi wa mabadiliko kwa faida ya jamii, mashirika yao na taifa kwa ujumla.
“Maendeleo binafsi ni matokeo ya motisha ya ndani. Mlifanya maamuzi ya kujifunza na kujiboresha. Mligeuza mambo mliyopaswa kufanya kuwa mambo mliyolazimika kufanya – jambo linaloonyesha uongozi wa kweli wa mabadiliko,” alisisitiza.
Aliwakumbusha kuwa viongozi wa aina hiyo huwa na malengo ya kuleta mabadiliko yenye maana, huku wakifungua uwezo wa timu zao kwa kuwasaidia wengine kufikia malengo yao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Kiongozi huyo aliwataka wahitimu kuendeleza uhusiano wao na UONGOZI Institute kupitia ushiriki wao katika programu mbalimbali kama vile elimu kwa wakuu wa taasisi, mijadala ya sera, tafiti, na uzalishaji wa maarifa.
“Jitokezeni kutoka katika maeneo yenu ya faraja. Kutana na wahitimu wengine, jengeni mitandao ya kitaaluma. Toeni utaalamu wenu kwa wanafunzi wa sasa, ikiwemo kuwa washauri wao,” alihamasisha.
Alisisitiza kuwa mitandao ya kijamii na kitaaluma ni nyenzo muhimu kwa maendeleo na ukuaji wa kitaaluma na kitaasisi.
Akihitimisha hotuba yake, Mhandisi Zena alikumbusha mafundisho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kusisitiza umuhimu wa kujiamini kama msingi wa maendeleo.
“Mwalimu Nyerere alitufundisha kujiamini hata tulipokuwa maskini. Changamoto iliyopo sasa ni kubadilisha imani hiyo kuwa siri ya mafanikio,” alisema.
Alisema kuwa kwa kutumia uongozi bora, Afrika inaweza kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zake za maendeleo.
Aidha, alieleza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, iliyozinduliwa mwezi uliopita na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa juu na kufikia pato la taifa la dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050.
Aliongeza kuwa dira hiyo inalenga uchumi unaojikita katika maarifa, viwanda na bidhaa za kuuza nje, sambamba na kuendana na ajenda za kikanda na kimataifa kama vile Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa.