NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Timu ya Taifa ya Tanzania, maarufu kama ‘Taifa Stars’ imeanza vyema kampeni zake katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa mwaka 2024 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Mchezo huo wa ufunguzi kwa kundi B umechezwa leo, Agosti 2, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliomiminika uwanjani, Taifa Stars meonesha kiwango bora cha mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho, wakitawala maeneo mengi ya uwanja na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu.
Ushindi huo umetokana na mabao yaliyofungwa katika vipindi viwili tofauti vya mchezo ambapo bao la kwanza lilifungwa katika dakika za lala salama za kipindi cha kwanza, dakika ya 45+3’, kupitia kwa mshambuliaji chipukizi anayekuja kwa kasi, Abdul Suleiman ‘Sopu’, ambaye aliipatia Stars bao la kuongoza kwa changamoto ya mkwaju wa penati.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa pande zote mbili huku Burkina Faso wakitafuta bao la kusawazisha, lakini walijikuta wakikumbana na ukuta imara wa ulinzi wa Taifa Stars na kuongeza bao la pili dakika ya 71 kupitia kwa beki wa kushoto Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Ushindi huo unaifanya Tanzania kuongoza kundi B kwa alama tatu, huku ikiwa imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya inayofata.
Kwa upande wake Kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amepongeza juhudi za wachezaji wake kuwa na nidhamu uwanjani, huku akiahidi kuendelea kupambana ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika michuano hiyo.
Mashabiki wa soka nchini wameonesha furaha kubwa kutokana na ushindi huo, wakiamini kuwa timu yao ina nafasi nzuri ya kufika mbali katika CHAN mwaka huu, ikizingatiwa kuwa mashindano yanafanyika nyumbani ambapo Taifa Stars inapata nguvu kubwa ya mashabiki.
Kwa ujumla, ushindi dhidi ya Burkina Faso umeleta matumaini mapya kwa wapenzi wa soka nchini, huku kikosi cha Taifa Stars kikiendelea kujipanga kwa mechi zijazo ili kuleta heshima kwa taifa.