Mkuu wa Kitengo cha Biashara Serikalini kutoka Benki ya NMB, makao makuu, Vicky Bishubo, amesema wamepanga kutumia maonesho ya wakulima Nane nane kutoa elimu kwa wananchi kutambua fursa zinazotolewa na benki hiyo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Bishubo, alisema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya wakulima kitaifa katika viwanja vya maonesho Nzuguni jijini Dodoma uliofanywa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
Alisema Benki ya NMB imejidhatiti kupanua wigo wa wadau waliopo katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itaongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.
“Mheshimiwa makamu wa Rais, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi pamoja na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuweka mazingira wezeshi kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
“Kwa lengo la kuongeza thamani na faida kwenye shughuli za kilimo, hivyo basi kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuchangia katika pato la Taifa,” alisema.
Aidha, alisema wanawapongeza washiriki wote ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa muitikio mzuri katika maonesho haya ya Nane Nane.
Alisema hiyo ni fursa nzuri kwa washiriki kujinadi, kubadilishana uzoefu na namna nzuri ya kukuza kilimo na pia kuweza kuona fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
“Na sisi Benki ya NMB tunawathibitishia kuwa tuko pamoja nao kuhakikisha wanasonga mbele zaidi,” alisema.
Kadhalika, alisema Benki ya NMB wanajivunia kuwa moja ya wadhamini wa maonesho haya ya Nane Nane mwaka huu 2025.
“Benki yetu imetoa mchango wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia maandalizi na ufanikishaji wa maonesho haya. Tunaamini kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, na tumejitolea kwa dhati kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta hii muhimu,” alisema.
Vile vile, alisema kwa kutambua kilimo kinahitaji uwekezaji wa kisasa hasa kwenye miundombinu wamekuwa na desturi ya kushiriki katika maonesho ya Nane Nane Kanda zote nchini wakiwa na mipango mkakati ya kuwezesha wafugaji, wavuvi na wakulima wa mazao yote ya biashara, ikiwemo Kahawa, Ufuta, Tumbaku, Korosho na mazao mengine ya chakula na biashara.
“Lengo letu ni kufikia wadau wengi zaidi. Ndani ya miaka mitano tumefungua zaidi ya akaunti milioni moja za wakulima, wafugaji na wavuvi nchi nzima,” alisema.
Pia, alisema wametoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi 100 bilioni kwa wafugaji nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Mbali na hilo alisema wamenunua na kunenepesha mifugo, kujenga miundombinu ya maji na mifugo ya kisasa yenye tija.
Pia, alisema kwa mazao mbalimbali kama kahawa wametoa mikopo ya shilingi bilioni 182, tumbaku shilingi bilioni 499, sukari shilingi bilioni 175 na shilingi bilioni 131 kwa zao la pamba.
Alisema wanawakaribisha wakulima, wafugaji sio tu kuchukua mikopo ya riba nafuu ili kuendeleza kilimo cha uhakika bali pia kupata elimu ya kisasa zaidi.
“Lakini pia tumeendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwapa wafugaji, wavuvi na wakulima wa Tanzania fursa ya kupanua uelewa kuhusu ufugaji na kilimo cha kisasa na hivyo basi kuwaongezea tija kwenye shughuli zao,” alisema.
Alisema pia NMB, wanayo huduma ya MshikoFasta ambapo mkulima kupitia NMB MKONONI anaweza kupata mkopo wa hadi shilingi 1,000,000 papo hapo bila dhamana yoyote kwa ajili ya shuguli za kilimo.
“Lakini pia kwa wakulima, tayari tunazo bima za hali ya hewa, bima ya mazao yaliyo shambani, bima za moto na wizi (kwa mazao yaliyohifadhiwa), bima kwa ajili ya vifaa vya kilimo na bima kwa ajili ya mifugo.
“Niwaombe tu wateja wa NMB na watanzania kwa ujumla kufika kwenye tawi lolote la NMB kupata huduma hii ya bima pamoja na bima zinginezo,” alisema.