Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Agosti 2, 2025
Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, ameomba tena ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo, akiahidi kuendeleza jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo na kushughulikia changamoto zilizobaki.
Aidha amesisitiza kuwa umoja wa wananchi ndio msingi wa kuendeleza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 15 ya uongozi wake.
Koka alitoa kauli hiyo katika mikutano ya kujitambulisha iliyofanyika Agosti 1 na 2, 2025 kwenye kata za Picha ya Ndege, Mkuza, Sofu, Msangani na Mailimoja, akiwa ameambatana na wagombea wengine watano wanaowania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wapo wanaouliza, ‘Koka atafanya nini tena miaka mingine mitano!!Jibu langu ni kwamba bado kuna kazi ya kukamilisha maeneo tuliyoanzisha, Changamoto bado zipo, kama maji, barabara, na umeme, lakini hatua zimekwisha chukuliwa serikalini na tunaamini zitamalizwa kulingana na bajeti,” alieleza Koka.
“Naomba ridhaa yenu, Tufike pale tulipoishia, tumeanza pamoja, tumefanikisha kuwa Manispaa, tushirikiane kumalizia changamoto zilizobaki,” alisema Koka huku akitoa mfano wa kata ya Sofu ambayo kwa miaka 15–20 iliyopita ilikuwa pori, lakini sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Aliahidi kuongeza nguvu katika usimamizi wa fedha za umma ndani ya Manispaa ili ziweze kutumika vizuri kutatua changamoto katika sekta muhimu kama maji, elimu, afya na barabara.
Kuhusu kero ya maji kwenye baadhi ya Kata alieleza , miradi ambayo ipo chini ya Serikali inaendelea kufanyiwa kazi kulingana na mikataba na anaamini mitihani hiyo itakuja kuwa historia kama ambavyo zilivyo kero ambazo zimeshatatuliwa.
Vilevile Koka, alieleza Katika bajeti 2025/2026 Manispaa ya Mji Kibaha tayari imeweka bajeti ya kushughulikia changamoto ya barabara ambapo imetenga kiasi cha sh.milioni 30 kwa kila kata.
Kwa mujibu wa Koka, Ushirikiano wake, madiwani ,Chama ,Serikali na Halmashauri, wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya baadhi ya barabara,sekta ya elimu ipo vizuri kwa kujenga shule mpya na nyingine kuzikarabati, zahanati, hospitali ya wilaya na soko la kisasa.
Kwa mujibu wa taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 3 Agosti kutafanyika vikao vya Kamati za Siasa za Kata na Wadi kwa ajili ya kujadili wagombea udiwani na kuwasilisha mapendekezo kwa Kamati ya Siasa ya Jimbo na Wilaya.
Agosti 4, 2025, wajumbe wa kila kata watapiga kura kumpata mgombea wa ubunge atakayewakilisha CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mbali na Koka, wagombea wengine wa nafasi hiyo kupitia CCM katika Jimbo la Kibaha Mjini ni Mussa Mansoor, Mwalimu Allawi, Charles Mwamwaja, Ibrahim Mkwiru, na Adv. Magreth Mwihava.