Na Meleka Kulwa , Dodoma
DODOMA, Agosti 2, 2025 –
Mgombea wa ubunge wa Viti Maalum Wanawake kupitia kundi la watu wenye ulemavu, Bi. Ummy Hamis Nderiananga, ameomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), ili aendelee kuwawakilisha kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Akihutubia wajumbe wa mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Bi. Ummy – ambaye amewahi kuwa Mbunge na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) – alisema anayo dhamira ya kuendelea kutetea haki na maslahi ya watu wenye ulemavu ndani na nje ya Bunge.
“Naomba kwa heshima na unyenyekevu ridhaa yenu ili niendelee kuwatumikia watu wenye ulemavu kupitia nafasi ya ubunge wa Viti Maalum Wanawake kwa kipindi kingine cha miaka mitano,” alisema Bi. Ummy mbele ya wajumbe wa mkutano huo.
Uchaguzi huo maalum wa UWT unaendelea leo jijini Dodoma, ukiwakutanisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kupiga kura na kuchagua wawakilishi watakaoliwakilisha kundi hilo maalum ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bi. Ummy ameahidi kwamba endapo atapewa nafasi hiyo kwa mara nyingine, ataendeleza juhudi za kuhamasisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati ya kuwalinda na kuwawezesha.