Balozi wa Indonesia, Bw. Tri Yogo Jatmiko, ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Kilimo yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma na kuelezwa majukumu ya DIB.
Balozi huyo alipokelewa na Meneja Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina ambaye alimweleza kazi ya DIB ya kukinga amana za wateja wa benki endapo taasisi zao zikianguka. Balozi huyo alieleza kufurahishwa na majukumu ya DIB.
Aidha, Balozi huyo alieleza uzoefu wa nchi yake ya Indonesia kwamba kinga kama hiyo hutolewa kwa wakulima juu ya mazao yao na kwamba endapo hawatapata mavuno mazuri, basi hulipwa fidia ya hasara yao na serikali.
Bodi ya Bima ya Amana inashiriki katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma na pia katika kanda, ambapo DIB iko katika kanda za Mashariki, Morogoro, Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya, Kanda ya Kaskazini jijini Arusha pamoja na Zanzibar.
Kauli mbiu ya Maonesho ya mwaka huu ni: Chagua Viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi. Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu ambapo watachaguliwa Rais wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na madiwani.