Na Silivia Amandius
KAGERA
Devota Daniel Mburarugaba na Samila Khalfan Amour wameibuka washindi katika uchaguzi wa Wabunge Viti Maalumu Mkoa wa Kagera baada ya kushinda kwa kishindo kati ya wagombea nane waliokuwa wakipigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoani humo.
Katika matokeo hayo, Devota Mburarugaba aliibuka kinara kwa kura 1,308, akifuatiwa na Samila Khalfan Amour aliyepata kura 1,250, na hivyo kutangazwa rasmi kuwa Wabunge wa Viti Maalumu watakaoiwakilisha Kagera.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Devota Mburarugaba alishukuru kwa imani waliyoonyesha wajumbe na kuahidi kushirikiana nao katika kuimarisha chama na kuhakikisha wanatafuta kura za kutosha kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Samila Khalfan Amour alisema ushindi huo ni ishara ya mshikamano wa wanawake wa Kagera na ameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza nguvu za chama na kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Kwa mujibu wa Katibu wa UWT Mkoa wa Kagera, Rehema Zuberi, jumla ya wajumbe 1,556 walishiriki kupiga kura katika uchaguzi huo, ambao ulisimamiwa na wasimamizi wawili na kuridhiwa na Kamati Kuu ya UWT Taifa.