NA DENIS MLOWE IRINGA
WAGOMBEA Watano kati ya Sita kutoka jimbo la Iringa Mjini wakiongozwa na waliokuwa wabunge katika vipindi tofauti mjini hapa Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge aliyemaliza muda wake Jesca Msambatavangu wameomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Iringa mjini kupitia CCM kila mmoja akielezea mafanikio aliyoyafanya katika kipindi cha utawala wake.
Akielezea Mafanikio akiwa Upinzani aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Simon Msigwa ambaye sasa ni kada wa CCM ameomba ridhaa kutoka kwa wajumbe katika kata nne walizotembelea kura za maoni kutoka kwa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mchungaji Msigwa, alisema licha ya kuwa katika chama cha upinzani kwa miaka mingi, alifanikiwa kutekeleza miradi kadhaa ya maendeleo kwa wananchi wa Iringa Mjini, ingawa alikumbana na changamoto nyingi kutokana na mazingira ya kisiasa ya wakati huo.
“Nikiwa upande wa mama wa kambo nilipambana kuhakikisha wananchi wanapata huduma, na sasa nikiwa ndani ya CCM chini ya mama mzazi naamini nitafanya zaidi kwa kushirikiana moja kwa moja na serikali,” alisema
Mbali na Msigwa, wagombea wengine wanaowania tiketi ya CCM kwa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini ni Fadhili Ngajilo, Wakili Moses Ambindwile, Islam Huwel, na Nguvu Chengula.
Wagombea wote wameendelea kujinadi mbele ya wajumbe wa kata mbalimbali, wakieleza dhamira na mikakati yao ya kuwaletea wananchi wa Iringa Mjini maendeleo endelevu endapo watapewa nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Jesca Msambatavangu, ameomba Ridhaa ya CCM Ashiriki Kinyang’anyiro cha Ubunge Iringa mjini iwapo watampa ridhaa hiyo, atahakikisha anakwenda kukamilisha miradi yote ya maendeleo ambayo aliaanzisha awali pamoja na kuibua mingine mpya.
Msambatavangu alisema nafasi hiyo akipewa ni kuendeleza yale mazuri aliyokwisha yafanya hivyo wasifanye makosa katika kumteua katika nafasi ya ubunge jimbo la Iringa mjini kwani amekishakomaa na amekuwa msemaji wa jamii katika matatizo Mbalimbali ya jimbo.
Naye Wakili Ambindwile akijinadi kwa wajumbe kupata ridhaa ya CCM Iringa Mjini alisema kuwa endapo atakuwa mbunge atatoa Msaada wa Kisheria Bure na Elimu ya Uchumi.
Ambindwile ambaye ni mwanasheria kwa taaluma, alisema endapo atapewa ridhaa hiyo na baadaye kuchaguliwa kuwa mbunge, ataweka kipaumbele katika kuwahudumia wananchi wa Iringa Mjini kwa kutoa msaada wa kisheria bila malipo kupitia ofisi yake ya sheria.
“Najua changamoto nyingi zinazowakabili wananchi, hasa katika masuala ya sheria, mikataba, migogoro ya ardhi na familia. Nitajitolea kuwasaidia bila malipo,” alisema.
Aidha, ameahidi kutoa elimu ya uwekezaji, fedha na uchumi kwa wananchi, ili kuwawezesha kuondokana na hali ngumu ya maisha, na hasa kuwaepusha na mikopo kandamizi inayojulikana kama “kausha damu” ambayo imekuwa kikwazo kwa wanawake wengi kwa sababu ya kukosa elimu ya kifedha.
Vile vile mtia nia Fadhili Ngajilo Akiomba Ridhaa ya Wajumbe CCM Iringa Mjini, Aliahidi Kuendeleza Huduma kwa Wananchi wa jimbo la Iringa kwa kuwa anajua vyema changamoto katika jimbo la Iringa mjini.
Ngajilo, ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Iringa kabla ya kuomba kupisha kwa muda nafasi hiyo kwa ajili ya kugombea ubunge, alisema ameomba ridhaa ya wajumbe hao kwa mara nyingine kutokana na nia yake ya dhati na wito wa kuwahudumia wananchi wa Iringa.
“Nina nia na malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Iringa mjini hivyo naomba nafasi ya uongozi kwa heshima ili niweze kugombea ubunge, si kwa sababu ya tamaa ya madaraka, bali kwa sababu ya wito na mapenzi niliyonayo kwa wananchi wa Iringa. Ninaamini nina uwezo, uzoefu na maono ya kuwatumikia kwa ufanisi,” alisema Ngajilo mbele ya wajumbe hao.
Mgombea mwingine Nguvu Chengula akiomba ridhaa alisema nafasi ya ubunge jimbo la Iringa mjini inamfaa kwa kuwa amekuwa mtu anayejitoa kwa jamii na chama nyakati zote hivyo wajumbe wajue mtu sahihi kwa sasa ni yeye.
Alisema kuwa mgombea anayefaa ni yule ambaye wakati wote amekuwa karibu na wananchi hivyo jamii inapenda kuwa mtu ambaye yuko karibu yao hivyo wajumbe wajifunze hilo.
Mgombea mwingine Islam Huwel akuweza kutokea kutokana na kile kilichoelezwa kuwa yuko katika kazi maalum hivyo kuwakilishwa na Katibu wa wilaya katika kuomba kura za wajumbe katika kuwania nafasi moja ya kuwania ubunge jimbo la iringa mjini.