Katikati ni mkuu wa mkoa wa Rukwa wakati akizungumza na watumishi wa idara ya afya
Picha na Neema Mtuka
……………
Na Neema Mtuka Kalambo
Rukwa: Vifo vya akina mama wajawazito katika Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kwa mwaka 2024 vimepungua kutoka vifo 8 hadi kufikia vifo 5 kwa mwaka 2025 .
Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali ya wilaya.
Taarifa kutoka idara ya afya wilayani humo imeeleza kuwa vifo vya Watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 38 kwa mwaka 2024 hadi kufikia vifo 9 kwa mwaka 2025 kwa kila vizazi hai 10000.
Aidha vifo vya Watoto wenye umri chini ya miaka 5 vimepungua kutoka vifo 45 kwa mwaka 2024 hadi kufikia vifo 11 kwa mwaka 2025 kwa kila vizazi hai 1000.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo Shafi Mpenda kupitia kikao cha Kujadili Sababu za vifo vya akina Mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto wachanga.
Ambapo Amesema kupungua kwa vifo hivyo kumechangiwa na serikali kuelekeza nguvu kubwa katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya na vituo vya kutolea huduma za afya.
Hata hivyo Takwimu za Utafiti wa Viashiria vya Huduma za Afya na Malaria (TDHS-MIS) wa mwaka 2022 zinaonesha kuwa kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini ni 104 kwa kila vizazi hai 100,000, wakati kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni 38 kwa kila vizazi hai 1,000.
Awali mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere akizungumza leoJulai 30,2025 katika kikao hicho amezitaka timu za usimamizi wa afya za wilaya kuhakikisha Kila kifo kinachotokea Cha mama mjamzito na mtoto mchanga kinachunguzwa kwa kina na kwa kuzingatia matakwa ya mwongozo wa ufuatiliaji na tathimini ya vifo kwa ajili ya kuchukua hatua.
“Vifo vya akina mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika ,havipaswi kabisa kuwepo katika Jamii yetu”amesema Makongoro.
Aidha amewataka wakurugenzi kuimarisha usimamizi madhubuti wa mfumo wa rufaa kwa wagonjwa kwa kuhakikisha magari ya kubeba wajawazito yanakuwa tayari kutoa huduma muda wote yanapohitajika.
“Tunawajibika kufanya kazi kwa mshikamanona ushirikianowa karibu kila mmoja kwa nafasi yake.”amesema.