Na Mwamvua Mwinyi – Pwani
30 Julai, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, amesema Mkoa huo unaandika historia mpya kupitia uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala na miradi mingine mikubwa ya kimkakati itakayofanyika Julai 31, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 30, 2025 katika eneo la tukio, Kunenge alieleza ,maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
“Tunaweka historia mpya mkoani Pwani, Huu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi wa viwanda na kuimarisha miundombinu ya kisasa,” alieleza Kunenge.
Alieleza Rais Samia atazindua Bandari Kavu ya Kwala, safari ya treni ya mizigo kupitia reli ya kisasa (SGR), mapokezi ya mabehewa ya MGR, na Kongani ya Viwanda ya Kwala – mradi mkubwa uliogharimu takribani trilioni 6.
Katika kongani hiyo, Rais Samia atazindua viwanda saba vilivyokamilika na kuanza uzalishaji pamoja na kutembelea viwanda vingine vitano vilivyopo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kunenge alieleza, safari ya treni ya mizigo kupitia SGR itazinduliwa rasmi katika Kituo Kikuu cha kuunganishia mabehewa ya mizigo na karakana maalum ya treni hizo maarufu kama Marchalling Yard ambayo ipo katika eneo la Kwala.
Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala, Kunenge alieleza mradi huo ,utaongeza ufanisi mkubwa kwa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na zaidi ya makasha 300,000 kwa mwaka hatua itakayopunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 30.
Aidha alieleza, Rais Samia anatarajiwa kupokea jumla ya mabehewa 160 ambapo mabehewa 100 ni mapya yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya reli ya MGR ,mabehewa 20 yamefanyiwa ukarabati na mabehewa 40 yametolewa na Shirika la Chakula Duniani WFP.
Faida zinazotarajiwa kutokana na miradi hiyo kuongeza pato la serikali, kukuza matumizi ya reli ,kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara kulinda mazingira na kuongeza ushindani wa kikanda na ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani zikiwemo DRC ,Zambia ,Rwanda, Burundi Malawi ,Zimbabwe, Uganda na Sudani ya Kusini.