Na Fauzia Mussa,
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta ya uvuvi na bahari kwa lengo la kusimamia kwa pamoja rasilimali za baharini na kuwezesha ushiriki wa wanawake na vijana katika Uchumi wa Buluu kote barani Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhandisi Omar Saleh Muhammed, wakati wa kufungua mkutano wa siku tatu wa kikanda kuhusu maendeleo ya sekta ya bahari uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Mhandisi Omar alisema kuwa maazimio ya mkutano huo yamelenga kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya bahari, kuweka sera jumuishi zitakazowawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uvuvi, pamoja na kuanzisha mifumo ya pamoja ya masoko na mitaji ndani ya jumuiya hiyo na bara la Afrika kwa ujumla.
“Tumejadili changamoto na fursa. Sasa ni wakati wa kuchukua hatua. Wanawake na vijana si walengwa tu bali viongozi wa mageuzi ya Uchumi wa Buluu Afrika,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo la mkutano lilikuwa kuona namna bora ya kutekeleza mradi wa miaka mitano unaolenga kuwawezesha wanawake na vijana katika bahari ya Hindi, ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinawanufaisha kwa vitendo wananchi walioko ukanda huo.
Aidha, alibainisha kuwa kundi la wanawake na vijana ndilo linalojihusisha kwa wingi na shughuli kama uvuvi, kilimo cha mwani na ufugaji wa viumbe baharini, hivyo Serikali itaendelea kuwapa mafunzo na nyenzo muhimu za kuwainua kiuchumi.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza kuwa hakuna mageuzi ya kweli katika Uchumi wa Buluu iwapo wanawake na vijana hawatashirikishwa kama viongozi wa mabadiliko.
Walisema ni muhimu kuanzisha mfuko maalum wa kuwawezesha, pamoja na vituo vya ubunifu na mafunzo ya teknolojia ya baharini.
“Kwa mara ya kwanza tumepewa jukwaa la kusikika. Tumepata mbinu mpya za ujasiriamali wa baharini na tutaondoka hapa na maarifa ya kubadili maisha ya jamii zetu,” alisema mmoja wa washiriki hao.
Ali Mabrouk Juma, mfugaji wa majongoo bahari kutoka Pemba, alisema mkutano huo umekuwa chachu ya mtandao mpya wa kitaalamu na ushirikiano na nchi nyingine. “Tumejifunza namna bora ya kusarifu bidhaa za baharini, kupata masoko ya kimataifa na kushiriki kwenye sera,” alisema.
Kwa upande wake, Salma Mwishaha Chato, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mikindani Seaweed na mshirika wa Kilimo Trust, alisema mkutano huo umeongeza fursa ya biashara ya bidhaa za baharini na kupanua masoko kupitia ushirikiano wa kimataifa.
Aliongeza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu thamani ya zao la mwani nchini Tanzania, na kuiomba Serikali pamoja na wadau kuendelea kuelimisha jamii kuhusu matumizi, ubora na masoko ya zao hilo.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, TradeMark Africa, Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), na Mastercard Foundation, ukiwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wavuvi, watafiti, watunga sera, wawekezaji na mashirika ya maendeleo kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Bahari Wafungwa kwa Maazimio ya Kuimarisha Ushiriki wa Wanawake na Vijana katika Uchumi wa Buluu