Na Silivia Amandius.
BUKOBA
Shirika la Cafe Africa, linalojihusisha na kilimo cha mazao, limeanzisha mradi mpya wa kuwajengea uwezo wakulima zaidi ya 35,000 wa kahawa mkoani Kagera. Mradi huu unalenga kuboresha ubora na kuongeza uzalishaji wa kahawa ili kufikia viwango vya soko la kimataifa na malengo ya nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika.
Meneja wa Cafe Africa, Samora Mnyaonga, alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi iliyofanyika kati ya 2020 na 2024 imesaidia wakulima kubadili mbinu za kilimo na kuongeza mavuno kwa kiasi kikubwa. Kutokana na mafanikio hayo, wafadhili wa kimataifa JDE Peet’s na Jacobs wametoa ufadhili wa awamu ya pili ya mradi kuanzia 2025 hadi 2029 ili kuendeleza maendeleo hayo.
Mradi huu mpya utaajiri maafisa ugani 500, viongozi wa wakulima 300, mashamba darasa 300 na wataalamu 200 watakaotoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alionyesha kuridhishwa na mpango huo na kueleza kuwa mkoa unalenga kuongeza uzalishaji hadi tani 200,000 ifikapo mwaka 2030. Aidha, mkoa umeanza kuwapa vijana 10,000 hekari moja moja za kahawa kama sehemu ya kuendeleza kilimo cha urithi na kuinua kipato cha kaya.
Meneja wa Bodi ya Kahawa Kagera, Edmond Zan, alisema kuwa serikali imetumia Sh bilioni 537 zilizotokana na mauzo ya kahawa, na kuhimiza wakulima kuzingatia ubora ili kufaidika na soko la dunia.