Waziri wakati Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania imeendelea kuongoza juhudi za kudumisha amani, usalama na ushirikiano wa kisiasa katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ Troika) katika kipindi cha kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025.
Waziri Kombo amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam, Balozi Kombo ametaja mafanikio kadhaa ambayo Tanzania katika kipindi cha uenyekiti wake, imeyapata ikiwa ni pamoja na kuandaa mikutano mikubwa ya kikanda, ikiwemo mikutano mitano ya Wakuu wa Nchi na Serikali za nchi wanachama kujadili masuala ya amani na usalama na Kuongoza Mkutano wa Tatu wa Maafisa Waandamizi wa Kamati ya Kisiasa na Kidiplomasia ya SADC, uliofanyika Dar es Salaam.
“Tanzania iliongoza Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu (SEOMs) uliofanyika katika nchi za Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia, iliratibu mkutano wa kihistoria kati ya Jumuiya ya SADC na Jumuiya ya EAC kuhusu hali ya usalama na amani Mashariki mwa DRC uliofanyika kwa mara ya kwanza na kuchangia vikosi katika jeshi la SADC lililopelekwa katika jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMI-DRC) lilipomaliza muda wake iliratibu urejeshaji wake kwa amani na utulivu,” alisema.
Kuhusu Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC (MCO), Waziri Kombo amesema mkutano huo utakaofanyika tarehe 24–25 Julai 2025 jijini Dar es Salaam utajadili hali ya ulinzi na usalama katika ukanda wa SADC, mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya SADC, mikakati ya kuzuia, kudhibiti na kutatua migogoro na uimarishaji wa mifumo ya tahadhari ya mapema ya kisiasa, kiusalama, kijamii na kiuchumi.
Amesema atauongoza mkutano huo kama Mwenyekiti na utawakutanisha wajumbe wapatao 300 wakiwemo Mawaziri na Maafisa Waandamizi wanaoshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, Ulinzi, Mambo ya Ndani na Usalama kutoka Nchi 16 Wanachama wa SADC. Mkutano huo ni miongoni mwa Mikutano ya ngazi za juu ya SADC, ambayo hufanyika mwezi Julai kila mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu amani, siasa na usalama katika nchi za ukanda wa SADC.
Mkutano huo unafanyika nchini kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo kuwa tarehe 18 Agosti 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo.