NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Khamis Mgeja amemshukia Balozi Hamphrey Polepole, akimtaka awaombe radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa kauli aliyoitoa yenye lengo la kukivuruga chama.
Mgeja alisema hayo wakati akitoa maoni yake kuhusu kauli ya Polepole ambaye pamoja na mambo.mengine alibeza utaratibu uliotumika kupitisha jina la Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa kiti hicho kupitia CCM.
Katibu huyo wa zamani wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, pia alibeza uteuzi wa Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza na alibeza pia uteuzi wa Dk. Hussein Ally Mwinyi kuwa mgombea pekee wa urais visiwani Zanzibar.
Mgeja ambaye yuko nchini India akipatiwa matibabu alisema Rais Samia, Dk.Nchimbi Dk Mwinyi ni wagombea halali kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu chama hicho kitapata ushindi wa kimbunga.
“Mimi Khamis Mgeja ni kada wa CCM, nimewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa Shinyanga na Njumbe wa NEC taifa, bado nipo nchini India kwa ajili ya matibabu. Pamoja na kwamba niko kwenye matibabu nimemsikiliza aliyekuwa Polepole akituhumu kwamba kuna mambo hayako sawa ndani ya chama na Serikali
“Na hasa kubwa zaidi analalamikia mchakato wa kuwapata wagombea urais kupitia mkutano mkuu wa CCM kwamba uteuzi wao haukuwa halali na ulinajisiwa kwa kuvunja Katiba na anasema hadi leo hajawapongeza wagombea hao.
” Kwangu mimi naona Polepole haijui vizuri Katiba ya chama na inawezekana hajawahi kuisoma zaidi ya kufahanu utamaduni na desturi za chama tu jambo ambalo amejidhihirisha kuwa haifahamu vizuri katiba ya CCM na kuitafasiri kwa usahihi,” alisema Mgeja
Aliongeza kuwa uelewa mdogo alionao Polepole katika masuala ya Katiba ndiyo yaliyomfanya ashindwe kutaja ni Ibara au kifungu gani cha Katiba kilichokosewa katika maamuzi ya mkutano mkuu kuteua wagombea urais.
“Polepole ameishia kusema tu desturi na utamaduni wa CCM haukufuatwa na kuzingatiwa huku ni kutoifahamu vizuri Katiba ya chama, napenda kumjulisha yeye na kikundi chake kilichojificha wafahamu kuwa taratibu zote zilifutwa na maamuzi yalizingatia matakwa ya katiba, wakasome mamlaka ya mkutano mkuu ibara ya 101 na 102 na vifungu vyake vidogo ndipo watakapojua uhalali wa maamuzi ya uteuzi wa wagombea hao,”
Mgeja alisisitiza kuwa uteuzi ulikuwa wa uwazi, majadiliano na mashauriano ya wazee wa chama yaliyotolewa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete yalikuwa bora kabisa.
Alimtaka Polepole na genge lake kutambua kuwa kama walikuwa na mgombea wao wa urais imekula kwao, watafute kazi nyigine ya kufanya na CCM itapata ushindi wa kishindo.
Alimsihi Polepole, aende katubu kwa upotoshaji na kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania.
Aidha Mgeja alisema Polepole anafanya kusudi kuwapotosha wananchi kwani anajua matakwa ya katiba inavyotaka anapofariki Rais.