Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa maafa wa wilaya ya Sumbawanga.
…………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya, Nyakia Ally Chirukile, amezindua rasmi mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa wajumbe wa kamati za wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuwa tayari kabla ya majanga kutokea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo leo Julai 22 yaliyofanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Menejimenti ya Maafa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).
Chirukile amesema kuwa maafa kama maporomoko ya ardhi, mlipuko wa kipindupindu, radi na ajali za majini yameathiri jamii na uchumi wa wilaya hiyo.
“Kuchukua hatua kabla ya majanga ni nafuu zaidi kuliko kushughulika na athari.,”amesema Chirukile
Amesema mafunzo haya ni nyenzo ya kuongeza ufanisi kwao katika kuzuia na kukabili majanga pindi yanapotokea.
Aidha amewataka wananchi kuacha tabia ya kujenga nyumba kwenye vyanzo vya maji na kuhama mabondeni ili kujilinda na maafa yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Kanali Selestine Masalamado kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maafa, amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, na yana lengo la kuwawezesha viongozi wa serikali za mitaa kuwa mstari wa mbele wakati wa dharura.
Naye mwakilishi wa UNDP, Clara Peter Maliwa, ameipongeza Wilaya ya Sumbawanga kwa kujitoa kikamilifu kushiriki mafunzo hayo na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya kukabili majanga nchini.
Baadhi ya wananchi wa mji wa laela akiwemo Sarah Makambi amesema ni muhimu elimu hiyo ikatolewa mara kwa mara ili wananchi wafahamu namna ya kukabiliana na majanga.
“Mara nyingi maafa yanatokea hususani majanga ya moto tunashindwa namna ya kudhibiti ila kwa elimu hii itasaidia kujikinga na maafa.” Amesema.
Mafunzo haya yamewaleta pamoja wajumbe wa Kamati Elekezi ya Maafa ya Wilaya na kamati ya Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, wakiwa na lengo la kujifunza mbinu bora za kupanga, kukabili, na kurejesha hali baada ya majanga.