Afisa Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Bi. Fatma Fungo, amepokea ugeni maalum kutoka kwa Miss World na Miss World Africa waliofanya ziara maalum katika kiwanda cha uzalishaji wa Tumaini Kits kilichopo Migombani, Unguja.
Warembo hao mashuhuri walitembelea kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya kujionea jitihada za ZMBF kupitia mpango wa Tumaini Initiative, unaolenga kuhakikisha kuwa wasichana balehe wanapata msaada wa bidhaa za afya ya hedhi ili waendelee na masomo yao bila vikwazo.
Katika ziara hiyo, Miss World alieleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na ZMBF na kupongeza juhudi za kuwainua wasichana kupitia elimu na huduma za afya. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika afya, elimu na ustawi wa mtoto wa kike kama njia bora ya kujenga jamii yenye usawa na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Bi. Fungo, zaidi ya wasichana 9,000 kutoka skuli mbalimbali za Unguja na Pemba wameshapatiwa Tumaini Kit, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika kipindi cha hedhi.
“Tumaini Initiative si mradi tu, ni harakati ya kuwajengea uwezo wasichana wetu na kuwapa fursa ya kutimiza ndoto zao bila kubaguliwa kwa sababu ya hali zao za kiafya,” alisema Bi. Fungo.
Ugeni huo umetajwa kuwa chachu ya hamasa kwa mashirika na wadau wengine kuunga mkono juhudi za kutoa elimu na huduma kwa mtoto wa kike visiwani Zanzibar na kwingineko.