Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Msumbiji alikutana na Mhe. Derrick Livune, Balozi wa Jamhuri ya Zambia – Msumbiji aliyefika Ubalozi wa Tanzania – Maputo kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni. Mkutano huo pia kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina nchi hizi mbili jijini Maputo, Julai, 22 20225.
Baada ya Salamu za Utangulizi, Mhe. Balozi Hamad alimkaribisha Mhe. Balozi Livune Jijini Maputo na kumhakikishia kila aina ya ushirikiano. Zaidi, alieleza kwamba uhusiano kati ya Tanzania na Zambia ni wa kihistoria na kwamba kumekuwepo na mwingiliano mkubwa wa watu wa nchi hizi kutokana na ukaribu wa kijiografia.
Mhe. Balozi Hamad poa aligusua miradi mbalimbali ya kimkakati na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta la TAZAMA na kutoa rai juu ya miradi hiyo kuendelezwa kwa maslahi ya Serikali na Wananchi wa nchi hizi mbili.
Kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi Kaskazini mwa Msumbiji na maeneo mengine Kusini mwa Afrika, Mhe. Balozi Hamad alisisitiza haja kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya SADC kushirikiana kwenye mapambanio hayo kwa kubadilisha taarifa (kuhusu mienendo ya ugaidi) na kudhibiti uingiaji holela kwenye maeneo ya mipakani kwa kuzingatia kwamba vitendo vya kigaidi havina mipaka.
Mwisho, alieleza jitihada za Ubalozi za kubidhaisha Kiswahili ambapo alitaarifu kwamba tayari umeanzisha mafunzo ya lugha hiyo kwa wafanyakazi wa TV na Redio Msumbiji na sasa upo kwenye hatua za mwisho kuanzisha Kituo cha Utamaduni (Culture Centre) ambacho pia kitatumika kufundishia Lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Livune alimshukuru Mhe. Balozi Hamad kwa kukutana naye na kutoa rai ya kuimarishwa uhusiano wa kirafiki na kihistoria uliokuwepo tokea wakati wa harakati za kupigania uhuru, uhusiano ulioasisiwa na Waazilishi wa Mataifa haya mawili, Hayati Mwl. Julius Nyerere (Tanzania) na Hayati Kenneth Kaunda (Zambia).
Kuhusu ushirikiano wa Kikanda, alisisitiza haja ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya SADC zenye Balozi nchini Msumbiji kufanya kazi kwa ukaribu ili kuhakikisha malengo ya Jumuiya hiyo yanatekelezwa. Aidha, alitoa rai kuhusu umuhimu wa wa kushiriki kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya hiyo yatakayofanyika Jimboni Nampula, tarehe 11 Hadi 17 Agosti, 2025.
Vilevile, alitoa ushauri wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa SADC TROIKA (kwa sasa) kuitisha mkutano wa Mabalozi wa SADC Troika waliopo Msumbiji (Tanzania, Malawi na Zambia) mwezi Agosti, 2025 ili kujadiliana masuala mbalimbali yanayoihusu Jumuiya hiyo, ushauri ambao uliungwa mkono na Mhe. Balozi Hamad sambamba na ushauri kushiriki kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya SADC Jimboni Nampula.
Mwisho, Balozi Livune aliupongeza Ubalozi wa Tanzania kwa jitihada za kubidhaisha Lugha ya Kiswahili ambayo kwa sasa ni miongoni mwa Lugha za Kimataifa na kupangiwa Siku Maalum ya kuadhimishwa kwake, tarehe 07 Julai kila mwaka.