Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 22 Julai 2025, amefungua rasmi Kikao cha Jukwaa la Kibunge katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa wa Mwaka 2025 kuhusu Maendeleo Endelevu _(Parliamentary Forum at the 2025 UN High Level Political Forum on Sustainable Development)_, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. Tulia ameeleza umuhimu wa Mabunge duniani kushirikiana kwa karibu na Serikali zao katika kujenga mifumo imara ya usawa wa kijinsia na afya kwa wote, sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususani Lengo namba 3 (Afya kwa Wote) na Lengo namba 5 (Usawa wa Kijinsia).
Akigusia Lengo la 3, Dkt. Tulia ameeleza kuwa bado kuna pengo kubwa katika upatikanaji wa huduma bora za afya, hasa katika nchi zinazoendelea, licha ya kwamba malengo haya yanatarajiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2030. Amehimiza haja ya ushirikiano madhubuti baina ya Serikali na Mabunge katika kuhakikisha kwamba huduma hizo zinaboreshwa na kufikika kwa wote.
Kuhusu Lengo la 5, Dkt. Tulia amesema licha ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika kupambana na ukatili, ubaguzi na ukosefu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, bado ipo kazi kubwa ya kufanya. Amesisitiza kuwa Mabunge yana wajibu wa kuendelea kutunga na kusimamia sheria zinazoimarisha haki, usawa, uwajibikaji na ufadhili wa kweli kwa mipango ya kuwawezesha wanawake na wasichana ili kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.