Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net) Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu wa Jeshi la Polisi CP Tatu Jumbe, amewaongoza Askari Wanawake kutoka Makao Makuu Dodoma pamoja na Watumishi raia katika kusherehekea siku ya Mtandao wa Polisi Wanawake maarufu kama TPF Net Gala Party 2025.
Sherehe hiyo imefanyika Julai 19,2025 katika ukumbi wa Polisi Jamii mkoani Dodoma, ambapo Kamishna Tatu Jumbe, amesema Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzani (TPF Net) uliundwa kwa lengo la kujenga uwezo wa kudumisha mshikamano miongoni mwa Polisi wanawake na jamii kwa ujumla ili kuimarisha mahusiano na kuwa karibu na wananchi na hatimaye kutoa huduma bora.
Akizungumza katika sherehe hiyo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni rasmi Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri, amewataka askari Polisi wanawake kuchangamkia fursa za kielimu ili kuongeza ujuzi, weledi na maarifa katika utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
TPF Net Gala hufanyika kila mwaka na huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo uwezeshaji wa kielimu, matendo ya huruma kwa kutembelea makundi yenye uhitaji na kujengeana uwezo na uelewa wa masuala mbalimbali ya kiutendaji, kijamii, afya na kiuchumi.