Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imetambua kipaji adimu cha mtoto Riziwani Martin Asheri, mwenye umri wa miaka 13, mkazi wa Kibaigwa mkoani Dodoma, ambaye ameonyesha uwezo wa kipekee katika kujenga barabara na madaraja, na kuahidi kumwendeleza ili kutimiza ndoto zake za kuwa mhandisi wa ujenzi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kusambaa kwa video fupi katika mitandao ya kijamii, ikimuonesha mtoto huyo akielezea na kuonyesha ubunifu wake katika sekta ya ujenzi, hali iliyowavutia watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, alielekeza Maafisa wa Wizara yake kwenda Kibaigwa kumtembelea mtoto huyo kwa lengo la kupata taarifa za kina kuhusu kipaji chake na historia yake ya maisha na elimu.
Katika ziara hiyo, Maafisa hao walizungumza na mtoto Riziwani, mama yake mzazi, mjomba wake pamoja na mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karume, ambao walieleza historia ya maisha ya mtoto huyo, mafanikio yake shuleni pamoja na ndoto zake za baadaye.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, Riziwani ana ndoto ya kuwa mhandisi maarufu nchini Tanzania na anataka kuchangia maendeleo ya taifa kupitia sekta ya ujenzi. Wizara imeahidi kuangalia namna bora ya kumsaidia kufikia ndoto hizo kwa kumwezesha kielimu na kitaaluma.
Hatua hii imepongezwa na wananchi na wadau wa elimu na maendeleo kwa kuonyesha kuwa serikali iko tayari kutambua na kuendeleza vipaji vya watoto tangu hatua za awali