Na Silivia Amandius
Kagera.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 9, ambapo awamu ya kwanza imepokea shilingi bilioni 4.6.
Ujenzi huo unatekelezwa na kampuni ya M/s Skywards Construction Company Limited kutoka jijini Dar es Salaam, ambayo imepewa jukumu la kujenga jengo hilo la kisasa kwa awamu mbili. Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la Kagambo, Kata ya Rwamishenye, Mkandarasi wa kampuni hiyo Bw. Haamid Ashraf ameahidi kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi ndani ya kipindi cha miezi 12, kama ilivyoainishwa katika mkataba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bi. Hajjat Fatma Mwassa alisema kuwa jengo hilo jipya ni sehemu ya maboresho ya mazingira ya utendaji kazi, na litasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Aliongeza kuwa jengo la sasa limepitwa na wakati, likiwa limejengwa zaidi ya miaka 60 iliyopita, na pia linakabiliwa na changamoto ya kujaa maji kutoka Ziwa Victoria kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mhandisi Raphael G. Nyatega kutoka ofisi ya Mkoa alieleza kuwa jengo hilo litaleta tija kubwa kwa wananchi na watumishi wa umma, sambamba na kuwavutia wawekezaji kutokana na nafasi ya kijiografia ya mkoa wa Kagera.
Ndugu Gozibert Kakiziba, Mkurugenzi wa kampuni ya M/s Goztecture (Mshauri Elekezi), alieleza kuwa usanifu wa jengo hilo umezingatia uimara, mvuto wa kisanifu, utunzaji wa uoto wa asili na kuakisi mamlaka ya serikali.
Mradi huo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha huduma kwa wananchi na kuboresha miundombinu ya kiutawala mikoani.