NA FAUZIA MUSSA
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman amesisitiza umuhimu wa watoa huduma za Msaada wa kisheria katika kukuza amani na haki hasa wakati taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Aliyasema hayo huko Ofisini kwake Mazizini wakati akitoa taarifa Kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sita ya wiki ya msaada wa Kisheria iliozinduliwa Leo na kufikia kilele chake Julai 18 mwaka huu.
Alisema tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi Mkuu watoa huduma za msaada wa Kisheria Wana mchango mkubwa katika kujenga amani na utulivu wa nchi.
Aidha Dk. Haroun alisisitiza umuhimu wa wiki hiyo katika kuimarisha haki, usawa, na utawala bora, akisisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Nafasi ya Watoaji wa Msaada wa Kisheria katika Kukuza na Kulinda Amani na Utulivu Zanzibar.”
Alieleza kuwa Kauli hiyo inalenga kuonyesha mchango wa watoa msaada wa kisheria katika kuhakikisha jamii inaishi kwa amani, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
DK. Haroun alibainisha kuwa kupitia elimu ya sheria, wananchi wanajengewa uwezo wa kutatua migogoro yao kwa njia ya amani na kuepuka michafuko.
“Watoa msaada wa kisheria ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanajua haki zao, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, na wanatatua migogoro kwa njia ya sheria badala ya vurugu,” alisema Dk. Haroun
Alieleza kuwa Katika wiki hiyo shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika zikilenga hasa kuwafikia watu walioko katika mazingira magumu wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Alizitaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na mbio za ngalawa zitakazofanyika Fumba, zikiwaleta wananchi pamoja kwa njia ya burudani na elimu ya kisheria.
Aidha alisema Jukwaa la Tano la Msaada wa Kisheria litafanyika Katika wiki hiyo likiwakutanisha wadau kujadili changamoto na fursa za sekta hiyo sambamba na Mikutano ya kijamii (outreach programs) itakayofanyika mjini na vijijini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kupata huduma hizo.
Alifahamisha kuwa Tuzo za Kitaifa za Watoa Msaada wa Kisheria zitazotolewa katika kilele cha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil, Kikwajuni mjini Unguja ambapo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayohudhuriwa na viongozi wa serikali, mashirika ya maendeleo kama UNDP, LSF, UNICEF, UN Women na wananchi wapatao 250.
Dk. Haroun aliyashukuru mashirika ya UNDP na LSF kwa mchango wao katika kuimarisha huduma ya msaada wa kisheria nchini na kuwasisitiza waandishi wa habari kushirikiana kwa karibu na Wizara katika kuhabarisha umma juu ya huduma hizo muhimu.
“Nyinyi ni sauti ya jamii. Tunaomba muendelee kushirikiana nasi ili kuhakikisha wananchi wote wanajua haki zao na wanapata msaada wa kisheria bila vikwazo,” alihitimisha Dk Haroun
Maadhimisho haya ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi. Hadi sasa, watoa msaada 283 wamewafikia wananchi zaidi ya 422,000 na kusikiliza malalamiko ya wananchi zaidi ya 400, yakiwemo masuala ya mirathi, stahiki za kazi, ardhi na ndoa.