Na John Bukuku – Dar es Salaam
Afisa Masoko Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bw. Andrew Punjila, amewashauri wadau wa maendeleo nchini kuhakikisha wanazitumia ipasavyo takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika kupanga programu na mipango ya maendeleo.
Akizungumza Julai 13, 2025, katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Bw. Punjila alisema kuwa takwimu hizo ni nyenzo muhimu kwa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuwa zinatoa mwongozo sahihi wa kuainisha mahitaji halisi ya jamii na maeneo ya kuwekeza.
“Takwimu hizi zinaonesha mwenendo wa pato la taifa, hali ya kiuchumi na fursa zilizopo kitaifa na kwa ngazi ya mikoa. Kwa mfano, kwa kutumia takwimu hizo, mtu anaweza kujua pato la mkoa kutoka mwaka 2012 hadi 2024, shughuli za kiuchumi zinazofanya vizuri, pamoja na hali ya pato la mtu mmoja mmoja,” alisema.
Aliongeza kuwa kupitia tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, wananchi na wawekezaji wanaweza kupata taarifa hizo muhimu na kuzitumia katika kupanga miradi ya maendeleo, uwekezaji na shughuli za kiuchumi kulingana na mazingira halisi ya kila mkoa.
Bw. Punjila alieleza pia kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kutumia takwimu za mazingira zilizokusanywa kupitia sensa, akibainisha kuwa bado matumizi ya mkaa na kuni ni makubwa, hali inayoonesha uhitaji wa elimu zaidi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuendana na juhudi za serikali za kutunza mazingira.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika nchini, ikiwemo ya Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi, itakayosaidia kubaini hali ya nguvu kazi kitaifa, kimkoa, kijinsia na kwa mujibu wa makundi ya umri.
“Tunaendelea pia na utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, ambao ni muhimu kwa serikali kutathmini hali ya ustawi wa wananchi, jitihada za kupunguza umaskini, na uwezo wa kaya katika kupata mahitaji ya msingi,” alieleza.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi kwa kutoa taarifa sahihi katika tafiti hizo utaiwezesha serikali kujua mafanikio na mapungufu katika utoaji wa huduma za jamii na kupanga mikakati ya kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mifumo ya Kijiografia kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Andrew Gondwe, alisema elimu ya takwimu inayotolewa kupitia maonesho hayo inawawezesha wananchi kubuni miradi ya maendeleo kulingana na hali halisi ya maeneo yao.
Alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kutumia taarifa hizo katika kupanga miradi na programu mbalimbali zenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.