Na Prisca Libaga RAS Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Kenani Kihongosi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kwake katika kufadhili, kuwezesha na kukuza vipaji na michezo mbalimbali nchini suala ambalo limekuza hamasa ya michezo nchini na kuibua fursa kwa Vijana wengi nchini Tanzania ikiwemo Vijana wa Mkoa wa Arusha.
Mhe. Kihongosi amebainisha hayo leo Jumapili Julai 13, 2025 wakati akiwa mgeni rasmi kwenye Fainali za pili za Mbio za pikipiki za Samia Motocross Championship, Mashindano yaliyoasisiwa na kuratibiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Christian Makonda.
“Nimshukuru kwa dhati na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye amedhihirisha kwa dhati ni mwanamichezo nambari moja. Serikali ya awamu ya sita iliwashika mkono vijana wa Pikipiki walioenda Morocco na tumeona amefanya kazi hii hata katika timu zetu za mpira ikiwemo goli la Mama ambalo liliongeza hamasa katika timu zetu kwenye michuano ya Kimataifa.” Amesema Mhe. Kihongosi.
Wakati wa utoaji wa zawadi kwa washindi wa vipengele mbalimbali zilizofikia takribani Shilingi Milioni 80 za Kitanzania pamoja na medali, Mhe. Kihongosi pia amempongeza Mhe. Makonda kwa ubunifu wake katika mashindano hayo, akisisitiza wajibu wa vijana wa Arusha katika kulinda amani, umoja na mshikamano ili kuendelea kufaidi mengi yanayosimamiwa na kutekelezwa na serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Kihongosi pia amewataka wananchi na hususani Vijana wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu ili kuitumia vyema fursa ya kuchagua viongozi bora na wachapakazi kwa mustakabali wa maendeleo yao na ya Mkoa wa Arusha.
Katika hatua nyingine Mhe. Kihongosi mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye Viwanja vya Lakilaki Kisongo, Mjini Arusha, amemvika Mhe. Makonda medali maalum kwaniaba ya wananchi wa Arusha, akimtakia Kheri Mtangulizi wake huyo na kumuahidi kuendeleza yote mazuri aliyoyaanzisha wakati akiwa Mkuu wa Mkoa huo.