NA DENIS MLOWE, IRINGA
CHAMA cha Mapinduzi Mkoani Iringa wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (MCC)Salim Abri Asas amewatembelea wahanga wa janga la moto lililoteketeza soko la Malimbichi la Mashine Tatu usiku wa kuamkia leo na kuzungumza nao katika utatuzi wa soko hilo.
Katika tukio hilo limeathiri ya wafanyabiashara 535 kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta na kuacha hasara kubwa kwa jamii ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Iringa.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MCC Asas ametoa pole kwa wafanyabiashara wote waliopatwa na janga hilo akieleza kuwa chama kimesikitishwa sana na tukio ambalo limeleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara hao.
Alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kipo pamoja na wananchi waliopatwa na janga hili na kinawajali sana kwani hali hii imewafanya watu wengi kuingia hasara kwani kuna baadhi yao walikopa sehemu mbalimbali hivyo wamekumbana na janga hili hivyo serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itawafuta machozi.
Aliongeza kuwa wakati huu ndio muda ambao wamachinga wanahitaji kuwa watulivu ili kuweza kupata tatuzi za kibiashara kutokana na janga hili watakaa chini kuweza kuangalia kutatua kwa haraka.
Aliongeza kuwa tayari mazungumzo yameanza kati ya CCM na Manispaa ya Iringa ili kujenga complex mpya katika stendi kuu ya zamani ili kuwawezesha wafanyabiashara kupata eneo lenye miundombinu bora na michoro ya awali ya ujenzi huo imeanza kufanyika.
Pia MCC Asas alisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini makini ya walioathirika ili kuepusha makosa kama yale yaliyotokea kwenye soko la Mlandege ambapo baadhi ya wahusika walikosa msaada licha ya kuathirika.
Kwa upande wa serikali, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta alisema kuwa tathmini ya awali inaonesha kuwa wafanyabiashara waliokuwa ndani ya soko ni 450 huku 85 waliokuwa nje pia wakikumbwa na athari.
Alibainisha kuwa serikali itaangalia namna ya kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika hasa wale walioko kwenye mikopo.
“Tunaelekeza BAKWATA kuhakikisha wanakuja na mpango kazi madhubuti ili kuruhusu biashara kurejea haraka lakini tunashauri biashara zihamishiwe kwa muda kwenye masoko ya Mlandege, Zizi, Ngome, Ipogolo na Magari Mabovu,” alisema DC Sitta.
Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa Musa Haruni alisema mamlaka hiyo ipo katika hatua ya kuchukua takwimu za walioathirika ili kupitia makadirio yao ya kodi na kuona namna ya kuwasaidia kutokana na athari walizopata.
“TRA imeelewa ukubwa wa changamoto tutaangalia namna bora ya kurekebisha makadirio ya kodi kwa kuzingatia hali halisi ya wafanyabiashara,” alisema Haruni.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Mwenyekiti wao, Jafary Sewando alieleza hali ngumu waliyonayo na kuomba serikali kuwasaidia hasa wale waliokopa mikopo kwa watu binafsi maarufu kama vimangara.
“Nguvu zote zimepotea. Tunaomba serikali isimame na sisi tunahitaji msaada wa haraka,” alisema Sewando.
Naye katibu wa BAKWATA Mkoa wa Iringa, Kabigili Said, alisema wamepokea maelekezo yote ya serikali na wako tayari kuyafanyia kazi akiiahidi kuwa BAKWATA itahakikisha eneo hilo linakuwa na miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara ili kurahisisha shughuli za kiuchumi.