Naibu Makamu Mkuu wa SUA anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa na Dkt. Naresh Jindal Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha LUVAS India wakitiliana saini hati za makubaliano ya ushirikiano wa kubadilishana wataalamu, Utafiti na mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo hivyo vya Kilimo Leo Julai 11, 2025 kwenye viwanja vya Saba Saba jijini Dar es Salaam.
……………
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeingia rasmi makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha (LUVAS) Haryana nchini India, yenye lengo la kuboresha elimu na teknolojia ya kilimo na ufugaji.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, yanajumuisha ubadilishanaji wa wataalamu, utafiti wa pamoja, maandalizi ya miradi na mafunzo kwa wakufunzi na watafiti wa pande zote mbili.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Naibu Makamu Mkuu wa SUA anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, alisema ushirikiano huo utasaidia Tanzania kupiga hatua katika matumizi ya teknolojia na kuboresha mifumo ya elimu ya juu, hususan katika sekta ya kilimo na ufugaji.
“Tunatarajia kupeleka wakufunzi wetu India, hasa katika hospitali za wanyama zinazomilikiwa na vyuo vyao. Kwa kuanzia, nafasi nyingi zitakuwa kwa Watanzania kwenda kujifunza huko, kwa sababu wenzetu wako mbele kiteknolojia,” alisema Prof. Muhairwa.
Aliongeza kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele ni sekta ya ufugaji, ambapo tayari SUA imeanza mchakato wa kupeleka madaktari wa mifugo India kujifunza mbinu za kisasa kama uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya chupa na uhamishaji wa mimba.
“Kwa sasa hatuna uwezo wa kuchagua jinsia ya ndama kabla ya kuzaliwa. Lakini kwa kutumia teknolojia ya India, ndani ya miaka minne hadi mitano tutaanza kuzalisha mbegu ambazo mkulima atachagua jinsia ya ndama atakayohitaji,” alifafanua.
Prof. Muhairwa alibainisha kuwa hali ya maisha ya vijijini ya Wahindi inafanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Watanzania, jambo linalotoa fursa ya kujifunza mbinu za kiteknolojia zinazoweza kutumika katika mazingira yenye changamoto zinazofanana.
“Kwa mfano, Wahindi wengi wanafuga ng’ombe wawili au watatu wakiwa mijini, lakini bado wanapata huduma bora kutoka hospitali za vyuo vikuu. Hii ni mfano mzuri wa kujifunza,” alisema.
Aidha, SUA imetoa protokali ya utambuzi wa magonjwa kwa kuku wa kienyeji, hatua inayolenga kuboresha usalama wa chakula na kukuza sekta ya ufugaji wa kuku nchini.