Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanikiwa kukamata kilo 11,031.42 za dawa mpya za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa katika kipindi cha Mei hadi Julai 2025.
Dawa hizo zilibainika zikiingizwa nchini kwa njia ya ujanja, ndani ya mifuko iliyokuwa na alama za mbolea.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam tarehe 9 Julai 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa dawa hiyo hatari inatokana na mmea wa Kratom na ina kemikali ambazo huathiri moja kwa moja mfumo wa fahamu wa binadamu.
Mitragyna Speciosa huonekana kama kichangamshi kwa mtumiaji, lakini pia huleta athari za kupooza fahamu, na kwa matumizi ya muda mrefu husababisha uraibu na vifo vya ghafla.
Kamishna Lyimo alieleza kuwa DCEA itaendelea kuimarisha udhibiti katika maeneo yote ya mipaka na kubaini mbinu mpya zinazotumiwa kuingiza dawa hizo nchini.
Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ili kuokoa jamii dhidi ya madhara makubwa ya kiafya na kijamii yanayosababishwa na dawa za kulevya.