Na Mwandishi wetu, Karatu Arusha.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-razaq Badru amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuiwezesha Mamlaka hiyo kufikia malengo iliyojiwekea katika mwaka wa fedha 2024/2
Akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa NCAA tarehe 9 Juni, 2025 Karatu Mkoani Arusha Kamishna Badru alieleza kuwa katika Mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka hiyo ilijiwekea lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 230 lakini ikavuka lengo hilo na kukusanya shilingi Bilioni 269.9 ambapo mapato yaliyokusanywa kutokana na shughuli za utalii ni Bilioni 262.74, mapato ya Pori la akiba Pololeti shilingi Bilioni 3.7 na mapato yaliyokusanywa kwenye vyanzo vingine vya mamlaka hiyo ni Shilingi Bilioni 3.274.
Aidha wageni wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro wameongezeka kutoka wageni 908,000 mwaka 2023/2024 hadi kufikia wageni 1,061,620 mwaka wa fedha 2024/2025.
Badru amewashukuru pia watumishi hao kuhamasisha upigiaji kura wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika kinyang’anyiro cha World travel awards na kuiwezesha hifadhi hiyo kutangazwa kuwa kivutio bora cha utalii Afrika mwaka (Africa’s leading tourist attractions 2025) katika tuzo zilizotolewa tarehe 28 Juni, 2025.
Amebainisha kwa kuwa sasa Mamlaka hiyo inaandaa mkakati wa miaka mitano ijayo ambapo mkakati utashirikisha kila mtumishi kujiwekea shabaha, malengo yanayopimika katika utendaji kazi na kubainisha kuwa mkakati huo utaendana na dira kuu ya taifa ya mwaka 2050 ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Mkakati wa NCAA utajikita katika kusimamia uhifadhi endelevu, kutangaza vivutio vya utalii na kuboresha miundombinu yote ya utalii ambayo inaenda sambamba na kuibua na kuendeleza mazao mapya ya utalii na pia mkakati utajikita katika shughuli za maendeleo ya jamii kwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Kamishna Badru amewasisitiza watumishi hao kuwa, ili kufikia malengo makubwa zaidi watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi, kutoa huduma bora na za viwango vya kimataifa kwa wageni, kuzingatia sheria na maadili ambapo vikifanyika kwa pamoja na kuweka mshkamano kwa watumishi wote itaiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma katika viwango vya kimataifa na kuendana na maono ya viongozi wa Nchi.