Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (wa tatu kulia) akikagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko wakati akiwasili katika miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mitambo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II.
…………..
NA NOEL RUKANUGU, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya nishati, ikiwemo kuanza ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Wilaya ya Chalinze hadi Kituo cha Kinyerezi III jijini Dar es Salaam, yenye urefu wa kilomita 135 na megawati 1,000. mradi ambao utasaidia kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika.
Akizungumza leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema Serikali inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miradi mikubwa ya kusafirisha umeme ili kuleta tija kwa Taifa.
Dkt. Biteko amesema kuwa awali kituo cha Kinyerezi III kilipangwa kuzalisha megawati 600, lakini hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya kuongeza uzalishaji wa umeme ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kwa watumiaji.
“Eneo la Mkuranga lina viwanda vingi hivyo linahitaji umeme wa kutosha. Katika baadhi ya maeneo kama Mkoa wa Katavi na Kigoma, wananchi walikuwa wakitumia mafuta kwa ajili ya uzalishaji wa nishati. Hata hivyo, hivi karibuni tumezima majenereta yaliyokuwa yakitumiwa na kuwasha umeme wa gridi ya taifa. Hali hii inaonesha kuwa mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko ameeleza kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji, ni lazima Serikali iendelee kuboresha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha huduma ya umeme wa uhakika inapatikana kwa wananchi wote.
Amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya nishati, ambapo kwa mwaka huu wa fedha, sekta ya nishati imetengewa bajeti ya Shilingi trilioni 2.3.
“Shauku ya Mhe. Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linafikisha umeme katika kila kitongoji nchini. Sisi kama watumishi wa sekta hii tunapaswa kuhakikisha ndoto hii inatimia kwa ufanisi mkubwa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa sekta ya nishati ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, na hivyo wafanyakazi wake wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa, huku akipongeza TANESCO kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake.
“Kwa sasa TANESCO inafanya kazi nzuri sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, tumeondoa utaratibu wa awali ambapo wateja walilazimika kupiga simu kwa gharama ili kupata huduma. Sasa huduma hizi ni bure – hatua kubwa ya kuboresha huduma na kuwafikia wananchi kwa karibu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2024, sekta ya Sanaa, Utamaduni, Michezo na Habari imekuwa kwa asilimia 17, huku sekta ya nishati ikishika nafasi ya pili kwa kukua kwa asilimia 14, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika miaka ya nyuma.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kulinda miundombinu ya umeme pamoja na kulipa gharama za matumizi kwa wakati ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutofuata utaratibu.