Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 9, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Dar es Salaam.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kuchochea kasi ya ushiriki wa makampuni ya Kitanzania katika shughuli za uchimbaji wa mafuta na gesi, kutoka chini ya asilimia 55 hadi kufikia asilimia 85.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 9, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba), yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema ongezeko hilo limetokana na uwepo wa makampuni mbalimbali ya ndani yanayojihusisha na ukusanyaji wa taarifa (data) ili kubaini maeneo yenye mafuta na gesi.
Mhandisi Sangweni amesema kuwa kampeni ya kwanza ya uchimbaji ilifanyika mwaka 2018 katika eneo la bahari kuu, ambapo kisima kimoja kilichimbwa na meli maalum iliyokuwa na wafanyakazi 150, kati yao Watanzania walikuwa 52.
“Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia idadi kubwa ya Watanzania wakihusika moja kwa moja katika kazi za uchimbaji, tofauti na zamani ambapo nafasi nyingi zilikuwa zinashikiliwa na wataalamu kutoka nje ya nchi. Hii imewapa Watanzania fursa ya kupata uzoefu wa moja kwa moja katika sekta hii,” amesema Mhandisi Sangweni.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna kampeni inayoendelea ya kuchimba visima vitatu katika mkoa wa Mtwara, huku akibainisha kuwa kazi zote zinazoweza kufanywa na kampuni za Kitanzania zimekuwa zikitolewa kwao kadri inavyowezekana.
Aidha, Mhandisi Sangweni ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo, hususan kupitia kuanzishwa kwa kozi za mafuta na gesi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuzalisha wataalamu wa ndani kwa ajili ya sekta hiyo muhimu.
Kuhusu ushiriki wa wananchi katika Maonesho ya Sabasaba, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kutembelea banda la PURA ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu sekta ya mafuta na gesi.
“Wananchi wengi wamekuwa wakitembelea banda letu na kuuliza maswali ya msingi kuhusu mafuta na gesi. Hili linaonesha ni kwa kiasi gani uelewa wa umma umeongezeka,” amesema.
Vilevile, amepongeza mwamko unaoendelea kushika kasi nchini kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku akisema kuwa ajenda hiyo imepewa kipaumbele kikubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni kinara wa ajenda hiyo si tu nchini, bali pia Afrika na duniani kote.