Na John Bukuku, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) na kupata maelezo kuhusu majukumu ya taasisi hiyo katika kulinda amana za wananchi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya katika banda la DIB Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba), Mhe. Kigahe alipokelewa na Bw. Nkanwa Magina, Meneja wa Uendeshaji wa Bodi ya Bima ya Amana, ambaye alieleza kwa kina jinsi DIB inavyotekeleza jukumu lake la kulinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Kigahe alipongeza kazi nzuri inayofanywa na DIB, hususan katika kuchangia utulivu wa sekta ya fedha nchini. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuendelea kutumia huduma za kibenki kwa kujiamini, wakifahamu kuwa amana zao zipo salama kupitia ulinzi wa Bodi hiyo.
“Bodi ya Bima ya Amana ni taasisi muhimu katika mfumo wa kifedha nchini. Inatoa hakikisho kwa wananchi kuwa fedha zao kwenye benki ziko salama hata pale benki inapopata changamoto ya uendeshaji,” alisema Mhe. Kigahe.
Kwa upande wake, Bw. Magina alibainisha kuwa DIB imekuwa ikishiriki katika maonesho haya kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya amana, ikiwemo taratibu za fidia endapo taasisi ya fedha itafutiwa leseni au kufilisika.
Alifafanua kuwa kwa sasa kiwango cha juu cha fidia ni hadi Shilingi milioni 7.5 kwa mteja mmoja kwa benki moja, na malipo hayo hufanywa kwa wakati bila usumbufu wowote kwa wateja wa taasisi husika.
DIB ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Amana (Sura 418), ikiwa na jukumu la msingi la kulinda amana za wateja wa taasisi za fedha, hivyo kusaidia kuimarisha imani ya wananchi katika sekta ya fedha na kuhimiza ushiriki mpana wa huduma za kifedha nchini.
Katika Maonesho ya mwaka huu, DIB imeendelea kutoa elimu kwa njia ya mabango, maelezo ya moja kwa moja, machapisho na ushauri kwa wananchi wanaotembelea banda lao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa kuhusu ulinzi wa amana za kifedha.