Na Sophia Kingimali.
Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole amesema toleo la Sheria ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili zinatarajiwa kuanza kutoka ifikapo Agosti mwaka huu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuagiza kutafsiriwa kwa sheria ili iweze kueleweka kwa urahisi na watu wa makundi yote.
Hayo ameyasema leo Julai 6, 2025 jijini Dar es salaam kwenye maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara mara baada ya kutembelea banda Mwandishi Mkuu wa Sheria lililopo kwenye maonesho hayo ya sabasaba.
Amesema kuwa sambamba na kuendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi hilo pia Ofisi hiyo imefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezeka na kuwafikia wananchi.
“Mpaka sasa tumefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha tunakuwa na sheria zinazowafikia wananchi kama Sheria na ukamilifu wake na lugha ambayo wananchi wanaifahamu” amesema Njole.
Ameongeza kuwa ofisi hiyo imefanya urekebu wa sheria mbalimbali ili ziweze kuendana na mahitaji ya sasa ya nchi “ tumefanya urekebu wa Sheria hizi kwa kuzikisanya sheria zote za nchi pamoja na kuingiza marekebisho ambayo yamekuwa yakifanyika kila wakati” amesema
Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kutengeneza mfumo wa sheria wa kusimamia matumizi ya Akili Mnemba (IA) na kubainisha kuwa mchakato huo utakapokuwa tayari utaandaliwa sheria.
Kwa upande wake Mwandishi Mkuu Msaidizi wa Sheria, Rehema Katuga amesema kuwa baada ya kukamilika kwa urekebu wa sheria mbalimbali ambazo zimeanza kutumika Julai mosi mwaka huu za awali hazitatumika tena.