Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendeleza, kukuza na kudumisha uhusian wa kidugu kati yake na Muungano wa Visiwa vya Comoro, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuimarisha mshikamano wa Afrika kupitia ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, mazingira na kidiplomasia.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Comoro zilizofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport, mjini Moroni.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema uhusiano wa Tanzania na Comoro haujajengwa kwa misingi ya mikataba ya kidiplomasia pekee, bali kwa moyo wa ujamaa, lugha ya Kiswahili, amani na imani ya pamoja.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kwa Tanzania, uhuru wa Comoro ni sehemu ya historia ya ukombozi wa Bara la Afrika, na amekumbushia namna Tanzania ilivyochangia harakati za ukombozi wa Comoro kupitia hifadhi kwa wapigania uhuru, msaada wa kifedha, kisiasa, uratibu na vyombo vya habari huku akitambua pia wanawake mashujaa wa nchi hiyo walioshiriki katika harakati hizo sambamba na wapiganaji wengine.
Halikadhalika, amepongeza mafanikio ya Comoro katika nyanja za uchumi, huduma za jamii, miundombinu na sekta ya utalii huku akimtaja Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assoumani kama kiongozi mwenye maono makubwa aliyeiwezesha Comoro kupiga hatua katika maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kuimarika kwa usafiri kati ya Tanzania na Comoro kupitia Mashirika ya Ndege ya Air Tanzania na Precision Air, pamoja na huduma za usafiri wa majini ni kielelezo cha dhamira ya kukuza muingiliano wa watu na biashara baina ya mataifa haya.
Mbali na hayo, Rais Dkt. Samia amebainisha mafanikio ya Comoro katika sekta za afya na fedha kupitia huduma za Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Benki ya Exim ya
Tanzania, zilizonufaisha wafanyabiashara na vijana wa nchini humo. Aliongeza kuwa Benki zingine kutoka Tanzania zipo njiani kuanzisha huduma zao nchini Comoro.
Katika kuimarisha uhusiano uliopo, Rais Dkt. Samia ameeleza utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Comoro kuwezesha ufundishaji wa Kiswahili katika shule nchini humo.
Akigusia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro katika kulinda ikolojia ya nchi zote mbili kwa faida ya vizazi vijavyo.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wananchi wa Comoro kuuenzi uhuru wao kwa kuimarisha mshikamano, haki, usawa na maendeleo jumuishi.
Shaaban Kissu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu