Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab ameshiriki katika Jukwaa la Mwanamke Hasina, kwa. niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Tabia Maulid Mwita huko Hoteli ya New Amani Complex Wilaya ya Mjini.
…….
Wilaya ya Mjini 06/07/2025.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka Waandishi wa Fasihi kumtizama Mwanamke katika muelekeo wa Maendeleo.
Akizungumza kwa Niaba yake, Fatma Hamad Rajab katika Mjadala wa wazi wa Mwanamke Hazina huko katika Hoteli ya New Amani Complex amesema Wanawake wanajipambanua sehemu mbalimbali kwa ajili ya Siasa na Biashara.
Hivyo amesema Mwanamke amekuwa ni mtu wa kubadili mtazamo kwa vitendo, ishara na uthubutu katika jamii.
Aidha amesema kutafakari nafasi ya Mwanamke ni tukio muhimu na inatakiwa kuthamini pamoja na kuenzi michango wa Mwanamke katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni hususan kupitia Fasihi ya Afrika.
Ameeleza kwamba, Mjadala huo, umetoa fursa ya kutafakari changamoto mbalimbali alizopitia Mwanamke katika nchi za kiafrika ambazo zilimdhalilisha na kuondosha utu wake.
Hata hivyo ametoa wito kwa Wanawake Nchini, kutobaki nyuma pamoja na kupambana ili kutimiza ndoto zao.
Amefafanua kuwa, Mwanamke ni daraja la kwanza katika kufundisha lugha, màlezi, makuzi ya mtoto na pia mlinzi wa maadili ya kiutamaduni katika Jamii.
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKIZA) Bi Consolata Mushi amesema tukio hilo ni dhamira ya kipekee ya kuenzi mchango wa Wanawake katika uongozi, Utawala na Maendeleo ya Jamii kwa kutumia lugha ya kiswahili ikiwemo Fasihi ya Afrika na nyenzo ya utambulisho wa Muafrika kwa ujumla.
Amesema Mwanamke Hazina ni muendelezo wa juhudi za kuhakikisha historia, sauti na mchango wa Wanawake katika Jamii zinatambuliwa kikamilifu .
Mbali na hayo amesema tukio hilo ni Jukwaa la kutafakari mafanikio, kujadili changamoto na kuibua mikakàti ya kushirikisha Wanawake katika nafasi za juu za Uongozi.
Jukwaa hilo la wazi ni miongoni mwa shamrashamra za kuelekea kilele cha Maadhimbisho ya kitaifa ya siku ya kiswahili Duniani, inatarajiwa kufanyika Julai 7 mwaka huu ambapo Mgenirasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.