GEITA
Imeelezwa kwamba katika kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Machi 2025 jumla ya shilingi bilioni 51.42 zilikopeshwa kwa wachimbaji wadogo wa madini 127 kutoka katika Taasisi mbalimbali za fedha nchini ikiwa ni juhudi za kuwapatia mtaji wachimbaji wadogo walio jisajii katika vikundi mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa leo Julai 6, 2025 na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wakati anafunga rasmi mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa wachimbaji wadogo wa madini 467 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia ujuzi ili kuongeza tija, usalama na ufanisi katika shughuli zao za uchimbaji madini.
Amefafanua kuwa, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo wa asilimia 40 ya maduhuli yatokanayo na uzalishaji wa madini nchini, hivyo itaendelea kuwajengea uwezo wa kila namna pamoja na kuendelea kuwapatia vifaa vya utendaji kazi kama itakavyohitaji.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Alana Nchimbi, amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi mwaka 2016, mpaka sasa, Serikali imetumia kiasi cha shilingi Bilioni 111.3 ambacho kimewawezesha wanufaika 157,909.
Aidha, ameongeza kuwa, kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 Serikali ilitenga jumla ya shilingi Bilioni 10.8 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hiyo ambapo jumla ya wanufaika 10,786 wamefaidika na 479 ni wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Geita, Bw. Titus Kabuo, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwa karibu na wachimbaji wadogo kupitia mafunzo ya ukuzaji ujuzi.
Amesema juhudi za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini zimeonyesha dhamira ya kweli ya kuwawezesha wachimbaji kufanya kazi kwa weledi.
Mafunzo hayo ya wiki moja yaliwashirikisha wachimbaji wadogo zaidi ya 200 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita. Washiriki walipatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu mbinu bora za utafutaji na uchimbaji wa madini, matumizi sahihi ya vifaa na kemikali, utunzaji wa mazingira, pamoja na afya na usalama kazini.