Na Mwandishi wetu, Babati
SHIRIKA lisilo la kiserikali la KINNAPA limeiasa jamii kuchangamkia vyema fursa ya kuwarejesha shule wasichana waliokuwa wamekatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.
KINNAPA katika kuhakikisha lengo hilo linatimia imefanikisha kuwarudisha shule watoto 200 ambao awali walishindwa kuendelea na msomo yao.
Mratibu wa KINNAPA, Abraham Akilimali ameyasema hayo mjini Babati mkoani Manyara, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Akilimali ameeleza kwamba kutokana na serikali ye awamu ya sita kutoa ruhusa kwa watoto wa kike waliokatiza masomo yao kurudi shule, jamii inapaswa kuchangamkia fursa hiyo.
Amesema shirika hilo isilo la kiserikali la KINNAPA, limefanikiwa kurejesha zaidi ya wanafunzi 200, hasa wasichana, mashuleni katika wilaya za Simanjiro, Kiteto, Babati mkoani Manyara na wilaya za Siha na Hai, mkoani Kilimanjaro, kupitia mradi wake wa “Mpe Nafasi”.
Akilimali amesema mafanikio haya yametokana na jitihada za pamoja kati ya shirika hilo, serikali, wadau mbalimbali wa maendeleo na jamii kwa ujumla.
“Kwanza kabisa tangu kuanza mradi huu wa ‘Mpe Nafasi’, tumerejesha watoto zaidi ya 200 shuleni, tumefungua na kujenga uwezo katika klabu zaidi ya 20 za wanafunzi, na tumeelimisha viongozi wa mila na dini pamoja na maafisa elimu katika wilaya zote tano,” amesema Akilimali.
Ofisa maendeleo ya jamii wa shirika la KINNAPA, Paulina Ngurumwa ameeleza kwamba wanafunzi hao waliorudishwa shule walikatiza masomo yao kwa vikwazo mbalimbali ikiwemo kupata mimba.
Ngurumwa ametaja changamoto nyingine zaidi ya mimba ni ndoa za utotoni au sababu nyingine ambazo zinazosababisha watoto kukatiza masomo yao.
Ofisa elimu wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Judith Materu, amesema pamoja na mafanikio hayo, bado changamoto za mimba za utotoni na ukosefu wa mahitaji muhimu zinawafanya wasichana wengi kushindwa kurejea au kubaki mashuleni.
“Kwa mwaka huu pekee, wanafunzi 21 wamerejea mashuleni hapa Babati, wasichana 10 na wavulana 11. Tunafanya kazi kwa karibu na wazazi ili kuhakikisha wasichana wanapata msaada wanaohitaji na jamii inaelewa umuhimu wa elimu,” amesema Materu.
Ofisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa Manyara, January Bikuba, amesema juhudi za pamoja zimefanikisha kupungua kwa visa vya ukatili wa kijinsia kutoka visa 330 mwaka 2022 hadi visa 293 mwaka 2024, huku visa 56 tu vikiripotiwa kuanzia Januari hadi Juni 2025.
“Kuna changamoto za unyanyapaa na hofu ya kulipiziwa kisasi, lakini tumeongeza huduma za msaada wa kisheria na madawati ya jinsia ili kusaidia waathirika,” amesema Bikuba.
Ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Mathias Focus, ametaja ukatili wa kiuchumi na kesi kumalizwa kifamilia kuwa changamoto zinazozuia juhudi za kukomesha kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
KINNAPA imewaasa waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kuendelea kusambaza taarifa kuhusu waraka wa elimu namba 2 wa mwaka 2021 na muongozo wa Februari 2022, unaosisitiza kurejeshwa shule kwa watoto wote walioacha masomo, hasa wasichana.
Mmoja kati ya waandishi wa habari walioshiriki kikao hicho Joseph Bura amesema watatumia kalamu zao katika kuhakikisha jamii hasa za wafugaji zinaendelea kuruhusu watoto wao hasa wa kike kufuatilia elimu ya watoto wao.