Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akiwa katika banda la mamlaka hiyo wakati alipotembela Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) leo Julai 5, 2025 jijini Dar es Salaam.
…..
NA NOEL RUKANUGU, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imejipanga kuendeleza utoaji wa elimu kwa wananchi kote nchini pamoja na kuendesha operesheni maalum za kuwakamata watu wote wanaojihusisha na biashara ya usambazaji na uzalishaji wa dawa za kulevya.
Imeeleza lengo ni kuhakikisha jamii inarejea katika mfumo bora wa maisha na kuwa na afya njema, jambo litakalosaidia kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo, Julai 5, 2025, kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa ushiriki wa mamlaka hiyo katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu aina mbalimbali za dawa za kulevya pamoja na kueleza masharti ya kisheria dhidi ya wahusika wanaokamatwa na dawa hizo.
Kamishna Jenerali Lyimo ameeleza kuwa kwa sasa DCEA inatoa elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
Aidha, mamlaka hiyo inaendelea na operesheni maalum za kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, wakiwemo wasambazaji na wazalishaji.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha ili wale wanaofanya biashara ya dawa za kulevya waache, wale ambao bado hawajajiingiza wasikubali kuingia, na waliokwishaathirika na matumizi ya dawa hizo wajue mahali pa kupata huduma na matibabu, ambayo hutolewa bila malipo katika vituo vyetu,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Ameongeza kuwa moja ya malengo makuu ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha wananchi wote wanarejea katika mfumo mzuri wa maisha na kuwa na afya njema ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Kamishna Lyimo amebainisha kuwa hali ya upatikanaji wa dawa za kulevya nchini imeendelea kuimarika kutokana na operesheni mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo, hali iliyosababisha dawa hizo kuadimika sokoni.