Arusha, 04 Julai 2025 –
Timu ya ukusanyaji mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ikiongozwa na Afisa Mapato wa Manispaa hiyo, leo imefanya ziara ya kikazi katika Jiji la Arusha kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa mapato.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa timu hiyo katika kutambua na kutumia vyanzo mbalimbali vya mapato, ili kuongeza ufanisi wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Kibaha. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambapo wataalamu kutoka Jiji hilo walitoa elimu juu ya mifumo bora ya ukusanyaji wa mapato, matumizi ya TEHAMA katika ufuatiliaji wa vyanzo, pamoja na mikakati ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Katika picha, timu hiyo ya Kibaha inaonekana ikifuatilia kwa makini mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi wao.
Mara baada ya mafunzo hayo, timu hiyo inatarajiwa kutembelea vivutio mbalimbali vya mbuga za wanyama vilivyopo mkoani Arusha kama sehemu ya kujifunza na kupata uzoefu wa namna sekta ya utalii inavyoweza kuwa chanzo cha mapato kwa halmashauri.