Na John Bukuku, Dar es Salaam
Katika jitihada za kuhamasisha ushiriki wa vijana kwenye maendeleo ya uchumi wa nchi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kutoa elimu ya fursa za kiuchumi kwa vijana wanaotembelea banda jumuishi la ofisi hiyo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuwafikia vijana kwa wingi na kuwaelimisha kuhusu mikopo na uwezeshaji unaotolewa na Serikali, ukiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na Mifuko mingine ya Uwezeshaji Kiuchumi.
Akizungumza Julai 4, 2025 alipotembelea banda hilo, Mhe. Ridhiwani alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwahusisha vijana moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji mali ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.
“Lazima tuhakikishe vijana wanapewa elimu ya kutosha kuhusu hizi fursa. Maonesho haya ni jukwaa la kufikisha taarifa na kuwahamasisha wachukue hatua. Tusiishie tu kutoa huduma – tuweke msisitizo kwenye elimu,” alisema Mhe. Ridhiwani.
Akiwaagiza maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zinazoshiriki katika banda hilo, Waziri huyo aliwataka kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa njia rahisi, ya kueleweka na kwa lugha rafiki ili kuwavutia vijana wengi zaidi.
Maonesho ya mwaka huu yamekuwa kivutio kwa taasisi nyingi za Serikali kutumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma na fursa mbalimbali, huku vijana wakipewa nafasi ya kipekee kutokana na mchango wao muhimu katika maendeleo ya nchi.