Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa akizungumza na wabunifu wa Chuo hicho wakati alipotembelea Banda Cha hicho leo Julia 3, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Chuo hicho katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere
……………
NA NOEL RUKANUGU, DAR ES SALAAM
Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, ili kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya sayansi pamoja na kuangalia ubunifu unaofanywa na wanafunzi wa chuo hicho, hususan katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza leo Julai 3, 2025 mara baada ya kutembelea banda hilo, Mkuu wa Chuo cha MNMA, Profesa Haruni Mapesa, amesema kuwa chuo hicho kimeanzisha sera inayoboresha mawazo ya wanafunzi, hali ambayo imechochea ubunifu wa miradi zaidi ya 30.
Amebainisha kuwa chuo kimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha bunifu hizo zinasajiliwa na kupata haki miliki ili ziweze kuingia sokoni na kuchangia maendeleo ya taifa.
“Tumekuwa na utaratibu wa kuwaunganisha wanafunzi wabunifu na taasisi kama Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), BRELA, na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili bunifu zao zisajiliwe rasmi na ziwe na tija,” amesema Profesa Mapesa.
Aidha, Profesa Mapesa ameeleza kuwa chuo hicho kinatoa elimu kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada za umahiri katika taaluma za sayansi ya jamii, pamoja na kufanya tafiti, kutoa machapisho yanayotokana na tafiti hizo. Pia, chuo hutoa ushauri wa kitaalamu na kozi za muda mfupi kwa wananchi.
“Tunatoa kozi mbalimbali katika sayansi ya jamii, tuna maktaba bora yenye machapisho na hotuba zote za Mwalimu Nyerere ambazo zililenga kuwaandaa Watanzania kupata uhuru na kuleta maendeleo ya kweli nchini,” ameongeza Profesa Mapesa.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilianzishwa rasmi Julai 29, 1961 kwa lengo la kuwaandaa viongozi wa Taifa watakaoliongoza baada ya uhuru. Chuo hiki kilianzishwa pia kwa heshima ya juhudi kubwa za Mwalimu Julius Nyerere katika kuelimisha wananchi na kuikomboa Tanzania.