Na Sophia Kingimali.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imetoa rai kwa viongozi wa dini nchini kutumia madhabahu zao kutoa elimu ya rushwa na kukemea kwa waumini wao ili kuzuia na kupambana na rushwa hasa kwenye kipindi hiki unapoelekea uchaguzi mkuu 2025.
Wito huo umetolewa leo julai 3,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Crispin Chalamila wakati akifungua warsha ya wadau kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu 2025 ambapo Julai 03, 2025 wamekutana na viongozi wa dini.
“Dini zetu zote zinakataa Rushwa na hata mafunzo ya mwenyezi Mungu mnayoyatoa huko yanatuonyesha jinsi rushwa Mungu alivyoizungumzia kuwa adui wa haki niwaombe bac mkiwa huko muwaelimishe waumini wenu madhara yatokana na rushwa”,amesem Chalamila.
Akizungumzia hatua zilizochukumiwa kwa upande wa serikali amesema Hadi sasa, Serikali imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki na usiogubikwa na vitendo vya rushwa.
Hatua hizo ni pamoja na Kutunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchagazi 2024 Kutunga Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2024,Kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa sura ya 278,Kuboresha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 ambapo sasa ina kifungu kinachotoa adhabu kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi na Kuiwezesha kimuundo, kimfumo na kiutendaji TAKUKURU ili, kwa kushirikiana na wadau wengine, iweze kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi.
Amesem rushwa katika uchaguzi wowote inadhoofisha misingi ya demokrasia na utawala bora kama ikiwa ni pamoja na kuvuruga uwapo wa usawa na ushindani baina ya wagombea kwa kutoa upendeleo kwa wagombea fulani lakini pia Inasababisha baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora (mfano uadilifu na uwajibikaji) kushindwa kugombea au kuteuliwa ama kutochaguliwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maaskofu na mashekhe,Askofu William Mwamalanga ameipongeza TAKUKURU kwa kuamua kushirikisha wadau mbalimbali katika vita dhidi ya rushwa hasa kwenye kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Amesema viongozi wa dini wananafasi kubwa kwenye mapambano hayo kwani hata wanasiasa na wananchi wote ni waumini wa dini hivyo watahakikisha elimu ya rushwa inawafikia.