Na Silivia Amandius, Biharamulo
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo nchini, Dkt. Gresmus Sebuyoya, amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kupitia tiketi ya CCM kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Dkt. Sebuyoya alipokea fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Biharamulo, Adamu Soud, katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za chama hicho. Tukio hilo limehudhuriwa na wanachama mbalimbali wa CCM waliokuja kushuhudia hatua hiyo muhimu ya mwanasiasa huyo ambaye pia ni daktari bingwa anayeheshimika kitaifa.
Akizungumza mara baada ya kupokea fomu hiyo, Dkt. Sebuyoya alieleza kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo ili kutumia taaluma na uzoefu wake wa kiuongozi kuchochea maendeleo ya watu wa Biharamulo Magharibi, hususan katika sekta za afya, elimu na uchumi. Alisisitiza kuwa wakati umefika kwa jimbo hilo kuwa na mwakilishi mwenye dira ya mabadiliko ya kweli.
Sebuyoya anakuwa mmoja kati ya watia nia 11 waliokwisha chukua fomu kuwania ubunge wa jimbo hilo, hali inayoashiria ushindani mkali ndani ya CCM kuelekea kura za maoni. Wakati harakati hizo zikiendelea kushika kasi, macho na masikio ya wakazi wa Biharamulo Magharibi sasa yanaelekezwa kwa wagombea hao wanaowania ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho tawala.