Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya marehemu 36 kati ya 42 waliopoteza maisha kwenye ajali mbaya ya magari iliyotokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa kuaga na kukabidhi miili hiyo kwa familia husika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Mhe. Babu amesema msiba huu ni pigo kubwa na tukio lisiloweza kuelezeka kwa maneno ya kawaida, huku akieleza kuwa viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wameguswa na msiba huo mzito.
Mhe. Babu amesema serikali inatambua machungu makubwa kwa familia ziliyosababishwa na ajali hiyo na kwamba kama ishara ya kuguswa na msiba huo, serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni tatu kwa kila familia iliyopatwa na msiba kutokana na ajali hiyo.
Aidha, Mhe. Babu amewasihi madereva wote nchini kuwa waangalifu barabarani na kuzingatia sheria za usalama wa barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga, amewataka wananchi wa Same kuendelea kushirikiana na kuwafariji wafiwa ili kudumisha upendo, umoja na mshikamano katika jamii hasa wakati huu wa majonzi makubwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameungana na waombolezaji hao na kutoa shukrani kwa wananchi, taasisi na wadau wote waliojitokeza kushiriki hatua za uokoaji na kutoa faraja kwa wafiwa.
Amesema ni uchungu mkubwa kwani wengi waliopoteza maisha anawafahamu binafsi na wamekuwa wakishirikiana nao katika majukumu mbalimbali ya maendeleo ya wilaya hiyo.
Ajali hiyo, ambayo imesababisha vifo vya watu 42 na kujeruhi wengine kadhaa, ilitokea baada ya basi la Kampuni ya Channel One lenye namba za usajili T 179 CWL lililokuwa likitoka Moshi kuelekea Tanga kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster lenye namba T 199 EFX lililokuwa likitokea Same kuelekea Moshi. Baada ya kugongana, magari yote yalishika moto na kusababisha vifo vya abiria waliokuwa ndani.