Dar es Salaam
Wakinamama wajawazito waliotembelea banda la Bohari ya Dawa (MSD) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, wamepatiwa zawadi ya mifuko yenye vifaa vya kujifungulia, ili kuwasaidia katika maandalizi ya uzazi salama.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa MSD, Bi. Etty Kusiluka, alisema kuwa pamoja na mifuko hiyo, wananchi pia wanapatiwa mipira ya kiume kama sehemu ya elimu ya afya ya uzazi na upangaji uzazi.
“MSD imejipanga kutoa elimu, kuonesha huduma zetu na kusambaza bidhaa mbalimbali za afya kwa wananchi wanaotembelea banda letu. Tumeshirikiana pia na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana ili kuwapatia wananchi huduma ya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu na kisukari,” alisema Bi. Kusiluka.
Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa maonesho hayo, tayari wananchi 170 wamepimwa afya zao na kupatiwa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu waliopo katika banda hilo.
Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na yanatarajiwa kufikia kilele chake Julai 13, 2025.