Dar es Salaam, Julai 2, 2025
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetia saini hati ya makubaliano na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu katika masuala ya kisheria na kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi wa sheria nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari alisema kuwa ushirikiano huo utalenga zaidi katika kutoa huduma za msaada wa kisheria, eneo ambalo bado lina changamoto kwa wananchi.
“Kama mnavyofahamu, LST ndiyo taasisi pekee yenye dhamana ya kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo. Imekuwa ikifanya kazi kubwa kwa Taifa letu, hivyo tumeona ni vyema kuendeleza ushirikiano huu kwa maslahi mapana ya nchi,” alisema Mhe. Johari.
Aliongeza kuwa kupitia makubaliano hayo, wanafunzi na wahitimu wa sheria watanufaika na mafunzo ya vitendo, huku wakishiriki moja kwa moja katika kutoa msaada wa kisheria kupitia vituo maalum vitakavyoanzishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kila mkoa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya LST, Prof. Sist Mramba, alisema makubaliano hayo ni fursa muhimu kwa taasisi hiyo kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wake.
“Wanafunzi wa LST wanapokuwa kwenye mafunzo ya uwandani huwa na utaratibu wa kutoa huduma za msaada wa kisheria. Kupitia ushirikiano huu, tutapanua wigo wa huduma hizo na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Prof. Mramba.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika sekta ya sheria na kusaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi, hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria.